Tanzania imeshinda
RAIS Dk Samia Suluhu Hassan amempongeza, Jihan Dimack kwa kutwaa taji la Miss Grand International 2026.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Instagram, Rais Dk Samia ameandika, “Ninakupongeza kwa dhati mwanangu, Jihan Dimack kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kutwaa taji la Miss Grand International 2026”.
Aliongeza: “Ushindi huu ni fahari kwa Taifa letu na kielelezo cha uwezo wa Watanzania kufikia mafanikio makubwa tunapoungana na kushirikiana. Pia, ni chachu kwa vijana, hususani wasichana, kujiamini, kuthubutu na kusimamia ndoto na vipaji vyao. Hongera sana. Ninakutakia kila la kheri”.
Jihan alitangazwa ni mshindi mkuu wa mashindano hayo ya kimataifa Oktoba 10, mwaka 2026 jijini Bangkok, Thailand.
Ushindi huo si tu kwamba umeitangaza Tanzania kwenye ramani ya dunia, bali umevunja mwiko wa miaka mingi kwa Jihan kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kutoka bara zima la Afrika kutwaa taji hilo kuu tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2013.
Ushindi wa Jihan umekuwa ishara ya nguvu ya ushirikiano wa Watanzania kupitia mitandao ya kijamii. Katika safari ya kusaka kura, hamasa kubwa ilitengenezwa mtandaoni wakiwemo watu mashuhuri na viongozi wa umma kujitosa usiku na mchana kuhamasisha wananchi kupiga kura.
Ushindi huo wa kihistoria wa Jihan kama Miss Grand International 2026 haukuwa tu matokeo ya urembo na akili yake jukwaani, bali kielelezo cha pekee cha nguvu ya umoja wa kitaifa na ushirikiano uliovuka mipaka ya Tanzania na kuitikisa dunia.
Kutoka kwa mabalozi wa urembo wa kimataifa waliopo ughaibuni, viongozi wa serikali, hadi kundi la vijana wa sasa (Gen-z), kila mmoja alisimama imara kuhakikisha bendera ya Tanzania inapepea kileleni jijini Bangkok, Thailand.
Miongoni mwa wahimizaji wakubwa wa mtandaoni alikuwa mrembo wa kimataifa, Miriam Odemba.
Mrembo huyo alikuwa na hamasa ya kipekee huku akifanya jitihada za kila namna akiwa safarini nchini Ufaransa, alionesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, “Nimejaribu kupiga kura kwa simu za watu wengine hapa Airport ya Paris na zinaingia. Kwa hiyo, nawaomba sana Watanzania wenzangu, hasa diaspora wetu waliopo Ulaya, tupaze sauti na tuungane kwa ajili ya Jihan wetu! Tuwafikie Watanzania wenzetu waliopo France, Spain, Italy, Germany na nchi nyingine zote za Ulaya. Kila mmoja ajitahidi kushiriki na kuhamasisha wengine kupiga kura kupitia njia rasmi. Tanzania ni moja, na umoja wetu ni nguvu yetu! Tumejitahidi sana, tusikate tamaa dakika za mwisho. Kila kura inayokubaliwa ni muhimu”.
Kushinda kwa Jihan kulifungua pia siri ya ushirikiano uliokuwepo nyuma ya pazia kati ya serikali na waandaaji wa hamasa hiyo.
Mshawishi na balozi wa hamasa ya ushindi wa Jihan, Jennifer Jovin maarufu kama Niffer, alieleza kuwa ushindi huo ulikuwa na mkono wa moja kwa moja kutoka kwa Rais Dk Samia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ambaye aliratibu mambo kimya kimya na kwa ufanisi mkubwa.
Niffer alieleza kuwa maua yote ya pongezi anayopewa yeye angetamani kumkabidhi Rais Dk Samia kwani msaada na msukumo uliotolewa na namba moja huyo wa nchi ulikuwa ni mkubwa mno na wa kihistoria.
Akizungumza kwenye video yake ya kwanza huku akitokwa na machozi ya furaha na hisia kali za ushindi, alihoji kwa hisia, “Wako wapi wale waliokuwa wanawabeza Watanzania? Watanzania kwa umoja wao wameshinda”.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa aliyekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kupiga kura na kununua tokeni za kura mtandaoni, alieleza kuguswa na mshikamano huo usio na kifani.
Katika ujumbe wake wa pongezi mara baada ya matokeo, Msigwa aliandika kwenye Instagram, “Watanzania wameshinda, Waafrika tumeshinda, tunaoipenda Tanzania tumeshinda. Asante Jihan Dimack. Hongereni wote mliosimama na Jihan mpaka mwisho, shukrani nyingi sana kwa Niffer balozi wa ushindi wa Jihan (umeonesha maana ya kuipigania nchi yako). Kwa Watanzania, ‘I’m speechless’ (Sina cha kusema). Heshima ya nchi inalindwa namna hii. Tushike hapo hapo. Umoja huu wa kitaifa umethibitisha kwa dunia nzima kuwa Watanzania wanapoweka nia na kushikamana, hakuna jambo linaloshindikana”.
Msigwa na Niffer walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha umma kupiga kura za mfululizo kwenye vipengele vya Nchi Yenye Ushawishi Mkubwa na Urembo duniani (Global Beauties Choice), hatua iliyofanya kila Mtanzania ajione kuwa sehemu ya ushindi huo mkubwa wa kihistoria.
Uzalendo huo wa kipekee ulipata pia pongezi za dhati kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima aliyesifu mchango wa vijana maarufu Gen-Z wa Tanzania na Afrika nzima walioratibu kampeni hiyo ya kura usiku na mchana.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dk Gwajima aliandika: “Vile nawaza uzalendo wa Gen-Z Tanzania kwa Taifa lao, maana kwa hili jambo la Jihan Dimack jinsi Gen-Z mlivyosimama imara kizalendo na kuratibu Gen-Z Afrika yote, haki mmetisha. Endeleni kusimama kizalendo daima na Mungu wa mbinguni atawapa heri zote. Gen-Z Oyeeeee na Gen-Z marafiki Afrika Oyeeee, Tanzania imeshinda, Afrika imeshinda! Huu uwe mwanzo wa ushindi zaidi popote inawezekana”.
Msisimko huo ulipamba moto zaidi mkoani Mwanza ambako ndiko Jihan alikotokea na kuiwakilisha Kanda ya Ziwa kabla ya kutwaa taji la kitaifa la Miss Grand Tanzania Agosti 8, 2026.
Wakati wakazi wa Mwanza wakilipuka kwa furaha wakijivunia kuwa binti aliyetokea katika mkoa wao ameiletea heshima Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Katika ukumbi maarufu wa The Super Dome uliopo Masaki, Dar es Salaam ulishuhudia mkusanyiko wa wadau wa urembo, wasanii na wananchi waliokusanyika kufuatilia fainali hizo mubashara kupitia skrini kubwa, na ukumbi huo ulilipuka kwa vifijo, nderemo na bashasha mara baada ya jina la Tanzania kutangazwa kuwa mshindi wa kwanza.
Katika ngazi ya kimataifa, ushindi huu umeipandisha Tanzania na kuifanya kuwa kitovu kipya cha urembo na mitindo duniani.
Jihan hakuwa tu mrembo aliyewania taji kwa sura, bali alidhihirisha dhana ya msingi ya inayohusu taji la urembo.
Dhana ya mrembo wa kisasa inazingatia misingi mikuu nne ikimwelezea mwanamke aliyekamilika kupitia mwili wake unaohusisha kuwa na afya njema, muonekano wa kuvutia na utimamu wa mwili.
Aidha suala la urembo ambao unaoangazia kuwa na sura nzuri, nidhamu ya hali ya juu pamoja na tabia njema.
Msingi wa tatu ni akili inayoeleza kuwa na elimu, uwezo wa kujieleza na uelewa mpana wa masuala mbalimbali, pamoja na biashara inayosisitiza kuwa na uwezo wa kujiendesha, mtazamo wa kijasiriamali na uwezo wa kubuni na kujenga fursa za kiuchumi.
Kupitia uwezo wake wa kujieleza na kutoa ujumbe mzito wa amani chini ya kampeni ya komesha vita na ukatili, Jihan pia aliibuka mshindi wa tuzo za ‘Grand Pageant Choice’ na ‘Golden Grand Award’ na hivyo kuthibitisha kuwa Tanzania ina amani na kusambaza ujumbe huo duniani kote.
Alipopewa nafasi ya kusimama kwenye jukwaa la dunia na kutoa hotuba yake kuhusu amani chini ya kaulimbiu ya Komesha Vita na Ukatili, Jihan aligusa hisia za majaji na watazamaji kote duniani kupitia mtiririko mzito wa maneno yenye busara na hekima.
Alianza kwa kueleza fahari yake kubwa ya kuzaliwa na kukulia katika taifa la Tanzania, nchi inayotambulika kote duniani kama kimbilio na kitovu cha amani, upendo na utulivu. Katika kuwasilisha msingi huo, Jihan alisisitiza kuwa nchini Tanzania amani siyo uhafifu au unyonge, bali amani ni ujasiri na ndiyo nguzo kuu inayowaunganisha watu wa tamaduni na asili tofauti kuishi kama familia moja.
Akiendelea na hotuba yake, Jihan alikemea kwa hisia kali madhara ya vita na vurugu duniani, akieleza namna migogoro inavyoharibu maisha ya watu wasio na hatia na kuteketeza ndoto za watoto na vijana.
Alitoa mwito kwa viongozi na jamii ya kimataifa kuchagua njia ya mazungumzo badala ya silaha, na kuwekeza kwenye huruma badala ya chuki, akihimiza kuwa kila mwanadamu anastahili kuishi kwa utulivu bila kujali utaifa, dini, au rangi yake.
Alipofika kwenye hatua ya maswali na majibu iliyohoji sifa za mwanamke mwenye ushawishi wa kweli, Jihan aligusa tena hisia za wengi kwa kueleza kuwa msingi mkuu wa amani na uongozi bora unaanzia kwenye kuwa na moyo wa utu na wema, akimtolea mfano mama yake mzazi kama kielelezo sahihi cha mwanamke anayewajali wengine na aliyejenga msingi wa amani na upendo katika maisha yake.
Safari ya Jihan hadi kufikia kilele hiki haikuwa ya siku moja.
Alianza ulimwengu wa urembo na ulimbwende akiwa na umri wa miaka 17, akishika nafasi ya tatu kwenye Miss Tanzania 2014, kabla ya kutwaa taji la Miss Universe Tanzania 2016 na kuiwakilisha nchi nchini Philippines mwaka 2017.
Akiwa na asili mchanganyiko ya Tanzania na Lebanon, na mwenye uzoefu wa kuishi nchi mbalimbali kama Msumbiji na China amerudi kwenye jukwaa la kimataifa akiwa na ukomavu na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 ambao hatimaye umempa heshima ya kuwa Malkia wa Urembo wa Dunia kwa mwaka 2026.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Thailand vimeelezea ushindi wake kama wa kihistoria huku wakimsifu jinsi alivyo Jasiri, mtulivu na anayejua nini anachokitafuta.
Magazeti na majukwaa makubwa ya habari nchini Thailand yalitoka na kichwa cha habari kinachoeleza ukubwa wa ushindi huo kwa Bara la Afrika.
Gazeti kubwa na mashuhuri nchini Thailand la The Nation Thailand limeandika historia mpya ya Tanzania na Bara zima la Afrika kufuatia kutawazwa kwa mrembo Jihan kuwa mshindi mkuu wa shindano la Miss Grand International 2026 jijini Bangkok.
Katika ripoti yake iliyoandikwa na mwandishi Nuttapakron Ngamsopa, gazeti hilo limebainisha Jihan aliibuka kidedea katika fainali hiyo iliyokutanisha warembo 80 nchi mbalimbali duniani.
Mrembo huyo wa Kitanzania alitwaa pia tuzo rasmi ya Kura za Mashabiki kutokana na kuonesha uwezo mkubwa uliowateka mashabiki wengi mtandaoni na ukumbini.
Habari hii ilitoka mara ya kwanza HABARI LEO

Post a Comment