SERIKALI YATAJA VIPAUMBELE VYA MPANGO WA MAENDELEO 2027/28 HUKU KAMATI YA BAJÉTI IKISISITIZA UBANAJI MATUMIZI




Serikali imewasilisha Bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2027/28, ukiwa na makadirio ya Shilingi trilioni 89.3 chini ya mfumo wa uwekezaji wa pamoja wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa uwiano wa 30 kwa 70. 

Mpango huo uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, unalenga kuendeleza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Dira ya 2050 kwa kujikita katika maeneo sita ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji jumuishi na uzalishaji wa ajira. 

Katika mwaka  wa fedha wa 2027/28, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kugharamiwa kupitia bajeti ya Serikali kwa kutenga Shilingi trilioni 20.7, wakati mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yatachangia Shilingi trilioni 6.3, na sekta binafsi ikitarajiwa kuwekeza Shilingi trilioni 62.3. 

Maeneo makuu ya kipaumbele yanayopewa uzito ni pamoja na kujenga uchumi imara na shindani, kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, kuendeleza vichocheo vya maendeleo kama nishati na miundombinu, kuchochea mageuzi katika sekta za kimageuzi, pamoja na kuimarisha misingi ya uendelevu wa taifa na utawala bora.  



 Wakati Serikali ikiwasilisha mpango huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki, imefanya uchambuzi wa kina na kutoa ushauri mzito kwa Serikali, ikisisitiza umuhimu wa kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kukabiliana na nakisi ya bajeti na kuongeza ufanisi. 

Kamati imependekeza kusitishwa kwa ununuzi wa magari mapya kwa mafungu yote isipokuwa yale yenye ulazima wa kipekee kwa mwaka mmoja, kupunguza gharama za shajala, kusitisha semina, warsha na michezo ya taasisi za umma kwa mwaka mmoja, pamoja na kuhakikisha kuwa taasisi zote ambazo bado hazijahamia makao makuu Dodoma zinafanya hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi mbili.   

Aidha, Kamati ya Bajeti imeiangazia sekta binafsi kama injini kuu ya uchumi na kushauri kuwa ili kufikia malengo ya kuchangia trilioni 62.3, Serikali lazima iweke kipaumbele cha dhati katika kuboresha mazingira ya biashara, kuharakisha utekelezaji wa sheria na mifumo ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), na kutatua changamoto za kimfumo zinazowakabili wawekezaji ili kulifanya taifa kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji wenye tija.   

No comments