MASWALI NA MAJIBU YA SERIKALI BUNGENI OKT 28: UWEZESHAJI, UJENZI NA MIKOPO



SERIKALI YATAJA MKAKATI WA KUKAMILISHA ZAHANATI ZA MASWA MAGHARIBI 

SWALI: Je, lini Serikali itapeleka fedha za kumalizia ujenzi wa Zahanati za Vijiji vya Nyashimba, Funika, Mandela, Nhelela, Kidema na Igwata zilizojengwa na Wananchi, kama alivyouliza Mbunge wa Maswa Magharibi, Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki?

JIBU: Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2018/19 hadi 2025/26, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imekamilisha ujenzi wa maboma sita (6) ya zahanati ya Isulilo, Jihu, Bukangilija, Nyabubinza, Mwang’anda na Mwabayanda ‘S’ kwa gharama ya jumla ya shilingi milioni 410. Aidha, alibainisha kuwa maboma 4 (Nhelela, Kidema, Funika, Mandela) yamepauliwa kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo na maboma 2 (Nyashimba ‘S’, Igwata) yapo hatua ya lenta.

Serikali imetenga shilingi milioni 100 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Isanga, na itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma yote yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kote nchini, yakiwemo maboma ya zahanati ya vijiji vya Nhelela, Kidema, Funika, Mandela na Igwata katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.

SERIKALI YAFANYA MAPITIO YA MWONGOZO WA USAJILI WA SHULE BINAFSI 

SWALI: Mheshimiwa Tamima Haji Abbas (Viti Maalum) aliuliza kama Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya masharti ya usajili wa Shule Binafsi nchini.

JIBU: Akijibu swali hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alieleza kuwa katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) na kuzingatia mabadiliko ya mahitaji ya sekta ya elimu, Serikali inafanya mapitio na kuboresha Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule wa Mwaka 2020. Hatua hizo zimewashirikisha wadau mbalimbali, akiwemo wamiliki wa shule zisizo za Serikali, ili kuhakikisha masharti yanaendana na hali halisi ya uendeshaji na mahitaji ya sasa.

Kupitia maboresho hayo, Serikali inalenga kurahisisha uwekezaji na kuweka mazingira wezeshi ya uanzishaji na uendeshaji wa shule binafsi bila kuathiri ubora wa elimu, usalama, na ustawi wa wanafunzi, sambamba na kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

SERIKALI YATOA MIKOPO NAFUU KWA WACHUUZI WA SAMAKI MWANZA 

SWALI: Mheshimiwa John Francisco Nzilanyingi (Nyamagana) aliuliza ikiwa Serikali haioni umuhimu wa kukopesha mtu mmoja mmoja na vikundi vya uchuuzi wa samaki katika mialo ya Jiji la Mwanza.

JIBU: Waziri wa Mifugo na Uvuvi alijibu kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwakopesha wafanyabiashara hao ambao ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani katika ukusanyaji, usafirishaji na uuzaji wa samaki. Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Serikali inatekeleza Programu ya Uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi kupitia Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu.

Katika awamu ya kwanza, jumla ya miradi 917 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.86 imewezeshwa nchini, ikiwemo miradi minane (8) yenye thamani ya shilingi milioni 74 kutoka Jiji la Mwanza, huku uchambuzi wa maombi 6,875 ya awamu ya pili ukiendelea, yakiwemo maombi 79 kutoka Jiji la Mwanza.

MIRADI YA MAJI 15 YATEKELEZWA KANGACHA KUTIMIZA DIRA YA TAIFA 2050 

SWALI: Mheshimiwa Martha Festo Maliki (Viti Maalum) aliuliza kuhusu mkakati wa Serikali wa kutekeleza Dira ya Taifa 2050 kwa kila mkazi wa Mkoa wa Katavi kupata maji safi nyumbani kwake.

JIBU: Akijibu swali hilo, Waziri wa Maji alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama. Kwa Mkoa wa Katavi, Serikali inatekeleza miradi ya maji 15 ya vijijini katika hatua mbalimbali za ujenzi, sambamba na mpango wa kufikisha maji kwenye vijiji vyote 1,575 nchini, ikiwemo vijiji 8 ambavyo havina huduma hiyo Mkoani Katavi.

Kwa upande wa mijini, miradi 5 inatekelezwa, wakiwemo mradi wa maji wa miji 28 katika Mji wa Mpanda kwa gharama ya shilingi bilioni 26 utakaofikisha huduma kwa asilimia 100, pamoja na kazi ya upembuzi yakinifu ya kutoa maji Ziwa Tanganyika kuhudumia mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi.

UHAWALISHAJI  TEKNOLOJIA NI TAKWA LA KISHERIA MIRADI YA MADINI MKAKATI

SWALI: Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko (Tarime Mjini) aliuliza kama kuna sera ya kulazimisha Technology Transfer Agreements kwenye miradi ya Madini Mkakati (Critical Minerals).

JIBU: Waziri wa Madini alijibu kuwa Sera ya Madini ya mwaka 2009 (Ibara ya 5.12), Kifungu cha 135 cha Sheria ya Madini (Sura ya 123), na Kanuni za Madini za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018 (Kanuni za 27 hadi 29) zinawataka wamiliki wa leseni za madini kuweka na kutekeleza mipango ya kuhamisha maarifa na teknolojia kwa wataalamu wa ndani.

Hivyo, uhawilishaji wa teknolojia ni takwa la kisheria katika miradi yote ya madini, yakiwemo madini muhimu na mkakati, na Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wake ili kujenga uwezo wa kitaalamu na kuongeza thamani ya madini nchini.

UJENZI WA WODI YA WANAWAKE HOSPITALI YA  SONGWE WAFIKIA ASILIMIA 80

SWALI: Mheshimiwa Juliana Shonza (Viti Maalum) aliuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuhakikisha ujenzi wa Wodi ya Wanawake katika Hospitali ya Mkoa wa Songwe unakamilika kwa asilimia mia moja.

JIBU: Akijibu swali hilo, Waziri wa Afya alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la wodi ya wanawake (Jengo la Mama na Mtoto) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe. Serikali imeingia mkataba na mkandarasi mpya ambaye ameanza kazi, ujenzi umefikia asilimia 80, na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2027.

MKAKATI WA SERIKALI KUDHIBITI TEMBO NA WANYAMA WAHARIBIFU  ITIGI

SWALI: Mheshimiwa Yohana Stephen Msita (Itigi) aliuliza mpango wa Serikali wa kudhibiti wanyama waharibifu hususan tembo wanaosababisha uharibifu wa mazao na mali Jimbo la Itigi.

JIBU: Waziri wa Maliasili na Utalii alijibu kuwa Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kuendelea kutumia kituo cha kudumu cha askari kilichopo Doroto na kambi za muda tatu (3) katika vijiji vya Chisingisa, Sanjaranda, na Kitaraka.

Juhudi nyingine zinazofanyika ni pamoja na kuimarisha doria, kutoa elimu, kugawa vifaa na nyenzo za kufukuza tembo ikiwemo ndege nyuki (drones), kushirikiana na wadau kama shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) kutengeneza vihenge 24 vya kuhifadhi mazao vilivyoboreshwa, na kuvuna tembo wawili (2) waliokuwa wakihatarisha usalama katika vijiji vya Doroto na Sanjaranda.

 

No comments