Serikali yaeleza namna inavyofufua netiboli
SERIKALI imeweka mikakati ya kufufua na kuendeleza mchezo wa netiboli kwa kuibua vipaji, kuwanoa makocha, waamuzi pamoja na kuwaandaa wachezaji kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Haya yalisemwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma wakati wa kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jasmine Ng’umbi.
Katika swali lake, Ng’umbi alitaka kujua mikakati ya serikali kurejesha uhai wa mchezo huo ambao kwa sasa umedorora. Mwinjuma alisema serikali inatambua umuhimu wa kuhuisha mchezo huo na inaendelea kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kuweka mikakati ya kuimarisha maendeleo yake.
Alisema hatua hizo zinalenga kuhakikisha mchezo huo unapata nafasi ya kukua, kuibua wachezaji wenye vipaji na kuongeza ushindani katika mashindano mbalimbali.
Aidha, Mwinjuma alisema pia serikali imeendelea “Mashindano haya ni miongoni mwa majukwaa muhimu ya kukuza vipaji na kuwapa wachezaji nafasi ya kuonesha uwezo wao, hatua inayoweza kusaidia kurejesha ushindani na hadhi ya mchezo huo nchini,” alisema.
Aidha, Mwinjuma alisema kupitia BMT, serikali imeendelea kuiwezesha Chaneta kushiriki mashindano ya kimataifa ili kuwapa wachezaji uzoefu na kuongeza uwezo wa kushindana na timu kutoka mataifa mengine, kuhamasisha ushiriki wa mchezo wa netiboli katika mashindano mbalimbali ya kitaifa, yakiwemo ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Mengine ni Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Kampuni Binafsi Tanzania (SHIMUTA), Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), Chama cha Michezo cha Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) na Shirikisho la Michezo ya Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania .
Alitaja mashindano hayo kuwa ni pamoja na Kombe la Netiboli la Afrika lililofanyika mwaka 2025 nchini Malawi na mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Netiboli kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 21, yaliyofanyika mwaka 2024 nchini Afrika Kusini. Aliongeza serikali pia iliwezesha Chaneta kushiriki mashindano ya Ligi ya Netiboli Klabu Bingwa Afrika Mashariki yaliyofanyika mwaka 2026 nchini Kenya na mwaka 2024 jijini Dar es Salaam. Katika hatua nyingine, alisema serikali iliwezesha chama hicho kugharimia uchaguzi wake uliofanyika Februari Mosi, 2026 jijini Dodoma.

Post a Comment