TANZANIA YAPATA FURSA NYINGINE ZA AJIRA 4,500 NCHINI QATAR
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania imepata fursa nyingine za ajira zaidi ya 4,500 kwa ajili ya Watanzania walio tayari kufanya kazi nchini humo kwenye kada mbalimbali.
“Tunatarajia kupata nafasi nyingine 4,500 kwa ajili ya Watanzania ambazo ziko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano ndiyo inaratibu zoezi zima kwa kushirikiana na wizara za kisekta ikiwemo ya Mambo ya Ndani pamoja na ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” alisema.
Tanzania imekuwa ikinufaika na fursa mbalimbali za ajira nchini Qatar ambapo hadi sasa kuna Watanzania 720 walioajiriwa kwenye Kampuni ya Taifa ya Usafirishaji ya Qatar (MOWASALAT) ikiwa ni sehemu ya nafasi za ajira 2,000 zilizotolewa katika awamu ya kwanza. Katika awamu ya pili, kampuni ya Power Holding International imetoa nafasi za ajira zaidi ya 4,000 kwa Watanzania wenye ujuzi mbalimbali.
Waziri Mkuu aliyasema hayo Septemba 28, 2026 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ziara yake ya siku tatu nchini Qatar na manufaa ambayo Tanzania imepata kutokana na ziara hiyo. Dkt. Mwigulu alikuwa nchini Qatar kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani.
Akielezea kuhusu mazungumzo yao, Dkt. Mwigulu alisema walijadili kuhusu hati mbili za makubaliano ambazo zilisainiwa jana hiyohiyo na wakaafikiana kwamba hati moja iliyobakia ya kuepusha ukwepaji wa kodi na utozaji wa kodi mara mbili ikamilishwe ili isainiwe mapema iwezekanavyo.
Hati zilizosainiwa jana ni Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo ya Zimamoto, Uokoaji na Huduma za Dharura baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Taifa la Qatar na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyingine ni Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kisiasa na Kidiplomasia baina ya Taifa la Qatar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ziara hii kimsingi ililenga kutilia mkazo maeneo yaliyokubaliwa na viongozi wetu wakuu wa nchi wakati walipokutana,” alisema.
Dkt. Mwigulu alitumia fursa hiyo kumwalika Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani afanye ziara nchini Tanzania ili kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili na kufuatilia utekelezaji wa mambo waliyokubaliana.
Alisema katika ziara yake alikutana pia na wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika mwaka 2022 nchini Qatar. “Lengo lilikuwa ni kupata uzoefu wao katika kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa na yakafanikiwa kwa kiwango cha juu sana. Hii ni fursa kwetu kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoandaa michuano ya Kombe la Mataifa Huru ya Afrika hapo mwaka kesho,” alisema.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alifuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Katibu Wakuu (OR-Uwekezaji), Wabunge na watendaji wengine wa Serikali.

Post a Comment