MUUNGANO: KATIBU MKUU DKT. ISLAM ASEMA MSINGI WA TAIFA HAUWEZI KUYUMBA
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum, amesema kuwa Muungano ni msingi muhimu wa Taifa ambao umeendelea kudumisha umoja, mshikamano, amani na ushirikiano kati ya wananchi wa pande mbili za Muungano.
Aidha amesisitiza kuwa muungano huo ni wa kipekee barani Afrika na duniani kwa ujumla na hauwezi kuyumba kwa kuwa ulianzia tangu zamani kabla ya kurasimishwa rasmi na waasisi wake.
Akizungumza Oktoba 2, 2026, wakati akifungua mafunzo maalumu kwa watumishi wa Idara ya Muungano mkoani Morogoro yaliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Islam amewataka watumishi hao kusimamia masuala ya Muungano kwa weledi, uadilifu na ufanisi.
Amesema kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali zote mbili Taifa limeendelea kutatua changamoto na kutoa fursa kwa watumishi kujifunza na kubadilishana uzoefu unaochochea kuimarishwa kwa Muungano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Muungano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Juma Mohamed Salum, amesema kuwa mafunzo hayo yataleta tija katika kuwajengea uwezo maafisa wa Idara ya Muungano kutoka ofisi zote mbili ili kutekeleza kwa ufanisi Mpango wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano, jambo ambalo litawawezesha wananchi kupata uelewa mpana wa masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano yanayotekelezwa kwa ushirikiano.
Dkt. Juma aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano, hivyo utoaji wa elimu hiyo utawasaidia kuelewa kwa kina historia na misingi thabiti ya muungano wa nchi yao.

Post a Comment