NDEJEMBI ATAKA UMEME KWA MKOPO KAMA MITANDAO YA SIMU




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametoa wito kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na sekta binafsi kuandaa mpango utakaowawezesha wananchi kununua umeme kwa mkopo unaofanana na mikopo ya mitandao ya simu.

Akizungumza katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya utiaji saini wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi kati ya Benki ya CRDB na TANESCO, Mhe. Ndejembi amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na mahitaji ya nyumbani hata wanapokabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Aidha aliiagiza Wizara ya Nishati na TANESCO kuendeleza mradi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuwaunganishia umeme kwa Shilingi 27,000 wananchi wanaoishi mazingira ya vijijini lakini mipaka ya kiutawala inawatambua kuwa wako mjini.

Aidha, ameeleza kuwa azma hiyo inalenga kufikia malengo ya kitaifa ya "Mission 300" na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, huku akipongeza ushirikiano huo thabiti kati ya taasisi za umma na sekta binafsi katika kutatua changamoto za wananchi.




Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono ya Dira ya Maendeleo 2050 na kueleza kuwa benki hiyo imedhamiria kuwa mshirika mkuu wa maendeleo kupitia uwezo wa kifedha, teknolojia, wataalamu na ubunifu katika kujenga uchumi imara na shindani.

 Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Razaro Twange, amesema upatikaji wa umeme nchini umezidi kuimarika huku nchi ikifikia uwezo wa kuzalisha megawati 4,500 hadi 4,600, ikiwa na mtandao wa kilometa 9,000 za kusafirisha umeme na zaidi ya kilometa 220,000 za kusambaza. 

Mkataba huo uliosainiwa leo utawezesha wananchi wa vijijini kuunganishwa umeme bure kupitia ruzuku ya Benki ya CRDB, wakati wa mijini wakiunganishwa kwa mkopo wa riba nafuu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

No comments