TRA YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO KWA MIEZI 27 MFULULIZO, YAKUSANYA TRILIONI 10.65




Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevuka lengo la makusanyo kwa miezi 27 mfululizo, ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 kuanzia Julai hadi Septemba, imefanikiwa kukusanya Shilingi trilioni 10.65 sawa na ufanisi wa asilimia 107.49 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 9.91. 

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ameeleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 18.81 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 8.96 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2025/2026, huku sehemu ya makusanyo kwenye Pato la Taifa ikifikia asilimia 15.80 ukilinganisha na asilimia 12.7 ya mwaka 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani.

Mwenda ameeleza kuwa mafanikio hayo yanatoa wastani wa makusanyo ya Shilingi trilioni 3.55 kwa mwezi kutoka wastani wa awali wa Shilingi trilioni 2.98, jambo linalowapa uhakika wa kulifikia na kulivuka lengo la makusanyo ya serikali kwa mwaka 2026/2027 la Shilingi trilioni 41.83. 

Katika kuongeza wigo wa kodi, TRA imesajili walipakodi wapya 447,611 kati ya Julai na Septemba mwaka huu na kufanya jumla ya walipakodi nchini kufikia 9,011,783 ikilinganishwa na walipakodi 8,564,172 waliokuwepo hadi Juni mwaka huu, sambamba na kuimarisha ufanisi wa uondoshwaji wa mizigo kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) uliowezesha kuingizwa kwa mizigo yenye thamani ya Shilingi trilioni 89.77, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 33.66.

Kuhusu udhibiti wa ukwepaji wa kodi na uingizaji wa bidhaa za magendo, TRA imekamilisha uchunguzi wa kesi zaidi ya 130 ambapo Shilingi bilioni 331.15 zilibainika na zaidi ya Shilingi bilioni 44.74 zilikusanywa, wakati kupitia doria 1,185 zilizofanyika katika mipaka yote ya nchi, bidhaa za magendo zenye thamani ya Shilingi bilioni 12.72 zilikamatwa na kodi ya Shilingi bilioni 5.34 ikakombolewa. 

Sambamba na hayo, Mamlaka imeendelea kuwezesha biashara kupitia Dawati la Kuwezesha Biashara kwa kutambua biashara 18,658 ambazo hazijasajiliwa, kuwezesha urasimishaji wa hiari wa biashara 10,778, kutatua changamoto za biashara 106 zilizokuwa katika hatari ya kufungwa, kulipa marejesho ya kodi ya Shilingi bilioni 419.15, pamoja na kutatua mashauri ya kikodi 10 nje ya mahakama yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.78 ili kulinda ustawi wa uwekezaji na biashara nchini.


No comments