HILI NDILO BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametangaza Baraza jipya la Mawaziri baada ya kukamilika kwa hatua za kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ikiwa ni pamoja na kumteua kiongozi wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar , Dk Mwinyi alisema uundwaji wa serikali hiyo umetokana na makubaliano ya maridhiano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo.
Alisema baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, pande hizo ziliunda kamati za pamoja zilizojadili na kufikia mwafaka kuhusu ajenda zilizokubaliwa.
Dk Mwinyi alisema pia alipokea majina ya Nassor Mazrui na Omar Said Shaaban kutoka ACT Wazalendo kwa ajili ya kujaza viti viwili maalumu katika Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Katika Baraza jipya, ACT Wazalendo imepewa nafasi nne za mawaziri, huku Dk Mwinyi akisema mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi wa serikali.
Akitaja baraza hilo jipya, alisema Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora itaendelea kuongozwa na Haroun Ali Suleiman, huku Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) ikiendelea kuongozwa na Hamza Hassan Juma.
Alisema Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo itaendelea kuongozwa na Riziki Pembe Juma, Ujenzi na Uchukuzi chini ya Dk Khalid Salum Mohamed, huku Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ikiongozwa na Dk Ado Mkoja Salum. Masoud Ali Mohamed ameteuliwa katika Ofisi ya Rais (Ikulu), akisaidiana na Shaaban Ali Othman.
Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi itaongozwa na Mudrik Ramadhan Soraga, Ardhi na Maendeleo ya Makazi ni Rahma Kassim Ali, Elimu na Mafunzo ya Amali na Lela Mohamed Musa, huku Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ikiendelea kuongozwa na Suleiman Masoud Makame.
Shariff Ali Shariff ataendelea kuwa Waziri wa Uwekezaji, wakati sekta ya Kazi imeondolewa katika wizara hiyo. Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu) itaendelea kuongozwa na Idrissa Kitwana Mustafa, huku Maji, Nishati na Madini ikiendelea kuongozwa na Nadir Abdulatif Yusuf Al-Ward.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaongozwa na Anna Athanas Paul, Fedha ni Saada Mkuya Akil huku Mipango ikihamishwa kutoka Wizara ya Fedha na kupelekwa Ofisi ya Rais.
Dk Mwinyi amemteua Nassor Mazrui kuwa Waziri wa Afya, Omar Said Shaaban kuwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Nasra Nassor Omar kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale.
Baada ya kupata ufafanuzi wa nafasi ambazo hazikutajwa awali, Dk Mwinyi alieleza kuwa Ali Suleiman Ameir ameteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji, huku Dk Mohammed Ali Suleiman, Mwakilishi wa Mtambwe kutoka ACT Wazalendo akiwa Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.
Kwa upande wa Naibu Mawaziri, Hassan Khamis Hafidh ameteuliwa Afya, Ali Abdalla Hussein Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Salha Mohamed Mwinjuma Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Zawadi Amour Nassor na Saif Kombo Pandu Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji na Dk Ahmad Omar Bakar, Kilimo.
Dk Salum Soud Hamed ameteuliwa na Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mohamed Saidjimine Mohamed ni Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Badria Ali Masoud apewa Ujenzi na Uchukuzi, Mboja Ramadhan Mshenga kapewa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Salum Ali yupo Maendeleo ya Jamii, Bakari Hamad Bakari ni Fedha na Juma Hassan Thabit Kaponda yupo Utalii na Mambo ya Kale.
Dk Mwinyi alisema Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji imepewa manaibu wawili kutokana na mgawanyo wa majukumu, mmoja akishughulikia Kazi na Ajira na mwingine Vijana na Uwezeshaji. Kuhusu utendaji wa SUK, alisema mfumo huo umeainishwa katika Katiba na sheria, na endapo kutatokea changamoto, Kamati ya Pamoja ya Mazungumzo itatumika kutafuta suluhisho na kudumisha maridhiano.
Dk Mwinyi pia alisema Zanzibar inaendelea na maandalizi ya Afcon 2027, akieleza kuwa ujenzi wa viwanja na barabara unaendelea na wakandarasi wanatarajiwa kukabidhi miundombinu hiyo Desemba mwaka huu.
Alisema serikali pia inaandaa mipango ya kuanzisha Shirika la Ndege la Zanzibar, Shirika la Reli na huduma za usafiri wa baharini kwa maboti maalumu ya abiria.

Post a Comment