BENKI YA DUNIA: UCHUMI WA TANZANIA WAENDELEA KUJENGEKA




Benki ya Dunia imesema uchumi wa Tanzania umeendelea kujengeka katika msingi wa utulivu na ukuaji, sambamba na kukua kwa ukusanyaji wa mapato huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa chini na deni la taifa likibaki himilivu.

Akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Tathmini ya Uchumi wa Tanzania yenye kaulimbiu ya ‘Kufanya Kazi Iwe na Tija’, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Firas Raad, alisema Tanzania imejenga misingi muhimu ya kiuchumi ambayo nchi nyingi zinazoendelea zingetamani kuwa nayo, huku uchumi ukikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.7 katika miongo iliyopita.

Raad alieleza kuwa utulivu huo unatokana na nidhamu ya kiuchumi ikiwamo udhibiti wa mfumuko wa bei ndani ya kiwango lengwa cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), usimamizi mzuri wa deni la taifa lenye hatari ya wastani, na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato. 

Pamoja na mafanikio hayo, tathmini hiyo inaonesha bado kuna changamoto ya ukuaji huo kutotafsiriwa kikamilifu katika kupunguza umaskini kwa kiwango kinacholingana, kwani sehemu kubwa ya ukuaji imejikita katika shughuli zinazozalisha ajira chache huku Watanzania wengi wakiwa katika ajira zenye uzalishaji mdogo.

Benki hiyo imebainisha kuwa kati ya ajira milioni 26 nchini, karibu ajira 550,000 pekee ndizo zenye ubora mzuri zikiwa na mshahara mzuri, mikataba na usalama wa kijamii, jambo linalotaka nguvu ielekezwe katika kuboresha ubora wa ajira na kuongeza uwekezaji kwenye mtaji wa rasilimaliwatu. 

Raad aliongeza kuwa wastani wa miaka ya masomo iliyorekebishwa kulingana na ujifunzaji nchini ni miaka 4.5, hali inayofanya uwekezaji katika rasilimaliwatu na miundombinu kuwa nguzo muhimu ya kufanya ukuaji wa uchumi kuwa mpana na wenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.


No comments