TanTrade kusimamia chapa ya Tanzania kwenye madini



MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imepanga kusimamia kampeni ya usajili na uwekaji wa chapa ya ‘Made in Tanzania’ katika madini yanayozalishwa nchini. 

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya matumizi ya chapa katika bidhaa zote zinazozalishwa nchini ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa taifa nje ya nchi. 

Meneja Ukuzaji Biashara wa TanTrade, Deo Shayo alitoa taarifa hiyo juzi wakati akizungumza katika kongamano la ‘Made in Tanzania’ katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita. 

Alisema kusudi la TanTrade ni kuona madini yanayozalishwa Tanzania yanatambulika kimataifa, kuipa nguvu chapa ya Tanzania, kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji. “Tunakusudia kuwaambia wazalishaji na wafanyabiashara wa madini wajisikie fahari kuyauza yakiwa na chapa hiyo. 

Shayo alisema madini adhimu ya tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee pamoja na mengine yanayozalishwa kwa wingi ni miongoni mwa yatakayopewa kipaumbele. 

Aliwaomba wafanyabiashara kuchangamkia usajili wa bidhaa zao kwa chapa hiyo akisisitiza kuwa mpaka sasa asilimia 85 ya huduma za TanTrade zinatolewa mtandaoni. 

Alisema kwa kipindi cha miezi 10 iliyopita, aina ya bidhaa 120 zimesajiliwa kwenye chapa ya taifa na hatua zaidi zinaendelea kuongeza mwamko na mwitikio katika kampeni hiyo. 

“TanTrade tutahakikisha tunaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa fursa za maonesho kwa kila aliyejisajili na Made in Tanzania tunatangaza bidhaa zao kupitia kanzidata yetu,” alisema. 

Aliongeza: “Pia, TanTrade itafungua kituo cha kimataifa cha biashara pale Ubungo, kwa kila aliyejisajili atapewa nafasi ya kutangaza sampuli ya bidhaa zake pale”. 

Mchambuzi wa Fedha, Kitengo cha Ununuzi wa Dhahabu, Kurugenzi ya Masoko ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Glory Maembe amesema benki hiyo imenunua tani 34 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 12.5, tangu mwaka 2024. Alisema mauzo ya madini yamefikia Sh trilioni 7.78 kati ya Januari na Juni 2026 sawa na asilimia 66.5 ya Sh trilioni 11.7 zilizorekodiwa katika mwaka mzima wa 2025, hali inayoashiria ukuaji mkubwa wa sekta ya madini.

No comments