Kustaafu kwa Bayi na mwelekeo mpya wa TOC

 



Kustaafu kwa Filbert Bayi baada ya kutumikia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa kipindi cha miaka 24 kama Katibu Mkuu kumehitimisha ukurasa wa kihistoria uliosheheni mafanikio, utumishi uliotukuka, na ujenzi wa misingi imara ya michezo nchini, jambo ambalo limewafanya wadau wengi kufurahishwa na maendeleo yaliyopo nchini huku wakikumbuka mchango wake mkubwa kwani kwa kizazi cha sasa kiongozi huyu alitwaa medali mbali mbali na kuipatia heshima Tanzania kimataifa, akitokea kwenye utumishi wa jeshi akiwa na cheo cha Meja na kuleta misingi ya uzalendo, uadilifu, na mapenzi ya dhati kwa taifa.

Kupitia uongozi wake, TOC ilipiga hatua kubwa katika kuimarisha maadili ya Olimpiki, kukuza mchezo wa haki, kutengeneza programu za utambuzi wa vipaji, na kuboresha utawala wenye uwazi na uwajibikaji, huku ikitambuliwa kuwa kazi kuu za TOC ni pamoja na kukuza na kulinda harakati za Olimpiki kwa kusambaza maadili ya urafiki, uelewano, usawa na mchezo wa haki nchini, kuandaa na kusafirisha timu za taifa katika mashindano mbalimbali ya kikanda na kimataifa, kukuza vipaji na elimu ya michezo kwa kushirikiana na vyama vya taifa, na kusimamia rasilimali na ruzuku zinazotolewa na IOC au wadau wengine ili ziwafikie wanamichezo kwa uwazi na uwajibikaji.

Katika mtazamo wa nadharia za maendeleo, hususan nadharia ya mtaji wa binadamu na maendeleo ya kitaasisi, uongozi wa miaka 24 wa Bayi unatoa masomo muhimu ya kujifunza na kukiendeleza ikiwemo utumishi wa kujitolea na uzalendo uliodhihirisha kuwa uongozi bora unasukumwa na mapenzi ya nchi badala ya maslahi binafsi.

Aidha, uadilifu na uwazi ulisaidia kujenga kuaminika kwa taasisi hiyo mbele ya serikali na jamii ya kimataifa, na utaalamu wa vitendo uliotokana na yeye mwenyewe kuwa gwiji wa riadha aliyeweka rekodi za dunia kabla ya kuhamia kwenye usimamizi wa kiutawala, mambo ambayo yanatakiwa kuendelezwa na viongozi wanaofuata ili kulinda hadhi ya michezo nchini.

Pamoja na hayo, kuna haja kubwa ya kumtumia Bayi kimkakati hata baada ya kustaafu kwake kwa kumteua kuwa mshauri mkuu au mlezi maalum ili kutumia uzoefu wake wa miongo mingi katika masuala ya diplomasia ya michezo ya kimataifa, kumtumia katika programu za kuwajengea uwezo wanariadha chipukizi na viongozi wapya kupitia ushauri nasaha na urithi wa maarifa, na kumtumia katika kusimamia ulinzi wa historia na tunu za taasisi hiyo ili misingi iliyowekwa isipotee wakati mifumo inapobadilika.

Wakati huo huo, mwenendo mpya na changamoto za michezo katika karne hii mpya unalazimu TOC kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia kwa kuzingatia sayansi ya michezo na uchambuzi wa data za kiutendaji badala ya kutegemea nguvu pekee, kuwekeza katika uchumi wa michezo kwa kuvutia uwekezaji binafsi na udhamini mkubwa utakaosaidia vyama vya michezo kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea ruzuku pekee, na kuimarisha utawala bora wa kidijitali katika usajili, ufuatiliaji wa vipaji na mawasiliano ya kitaasisi ili kuongeza ufanisi, kuboresha ushindani wa kimataifa na kuvutia vijana wengi zaidi kushiriki katika shughuli za maendeleo ya michezo nchini.

Tathmini hii linaonyesha kuwa mafanikio ya Filbert Bayi ndani ya TOC hayapaswi kuonekana kama ukurasa ulioufungwa bali ni dira na mwongozo thabiti wa namna ya kuendesha taasisi za michezo kwa uadilifu, uzalendo, na maono ya mbali.

Ili Tanzania iweze kupiga hatua kubwa zaidi katika medani za kimataifa, ni lazima iunganishe tunu hizo za kizalendo na mifumo ya kisasa ya kisayansi na kiuchumi, huku ikihakikisha rasilimali watu nguli kama Bayi zinaendelea kutumika kama nguzo ya ushauri na urithi wa kitaifa kwa kizazi cha sasa na vijavyo.


No comments