ULINZI WA BAHARI SASA USIPIME
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa
Palamagamba Kabudi amesema Sh bilioni 5.8 zimetumika kukamilisha mradi wa
kuimarisha ufuatiliaji wa ulinzi wa bahari katika maji ya Pwani ya Tanzania
kufuatia athari za mgogoro wa Bahari Nyekundu.
Pamoja naulinzi
uwepo wa mradi huo unatatua changamoto za kiusalama na kukuza maendeleo kwa
wananchi.
Akieleza
kuhusu mradi huo ulioanza Machi 2025 na kukamilika baada ya uzinduzi wa boti
mbili za doria zenye mwendokasi mkubwa ziitwazo PB Sailfish 2 na PB Sailfish 3,
Profesa Kabudi alibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kukabiliana na uhalifu
katika mwambao wa Pwani uliosababishwa na ongezeko la mashambulizi ya
wanamgambo wa Houthi katika Bahari Nyekundu yaliyotishia usalama wa meli na
kuongeza gharama za usafirishaji.
Mbali na
boti hizo zenye uwezo wa kubeba watu 12 kila moja na kufika Zanzibar kwa nusu
saa pekee, Profesa Kabudi alieleza kuwa mradi huo ulijumuisha mafunzo ya
kuwajengea uwezo vikundi vya wakulima wa mwani, ujenzi wa kaushio la mwani, na
ununuzi na usambazaji wa mashine za kusaga mwani kwa ajili ya kuongezea thamani
mazao yao katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Makamu
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa Provident Dimoso
alibainisha kuwa chuo hicho kilisimamia ununuzi wa boti hizo kwa kuzingatia
sheria za umma na viwango vya kimataifa ambapo boti hizo ziliharimu Sh bilioni
4.2 zikiwa na uthabiti wa hali ya juu, mifumo ya kisasa ya urambazaji na
mawasiliano kwa ajili ya doria na operesheni za uokoaji.
Naye
Balozi wa Japan nchini, Mikami Yoichi alipongeza hatua hiyo na kueleza imani
yake kuwa serikali ya Tanzania itahakikisha boti hizo zinatumika kwa ufanisi na
zinatunzwa ipasavyo ili ziweze kuleta tija kwa taifa kwa miaka mingi ijayo.

Post a Comment