Shinyanga yahimizwa amani kupitia utamaduni
WAKAZI wa Shinyanga wamehimizwa kutunza amani ili waendelee kufurahia utamaduni wao na kuendeleza mshikamano uliopo miongoni mwa jamii.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano linalofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, ambalo linahitimishwa leo.
Njange alisema amani ni msingi muhimu unaowawezesha wananchi kusherehekea na kuenzi utamaduni wao kwa uhuru, huku wakikumbuka walikotoka, walipo sasa na wanakokwenda kama jamii.
Alisema tamasha hilo ni sehemu ya kuimarisha umoja na kuonesha kuwa Tanzania ni nchi yenye utulivu, mshikamano na utajiri mkubwa wa tamaduni mbalimbali.
“Nawashukuru wananchi wote kwa kufika kwenye tamasha hili la utamaduni wa Msukuma, nawaomba mwendelee kujitokeza kwa wingi ili kwa pamoja tusherehekee utamaduni wetu,” alisema Chifu Kidola wa Pili.
Tamasha hilo linatoa fursa kwa wananchi kushuhudia ngoma za asili, maonesho ya biashara, pamoja na michezo mbalimbali ya watoto.
Kwa upande wake, Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Shinyanga, Innocent Mtafi alisema tamasha hilo lina mchango mkubwa katika kuhifadhi, kuenzi na kuendeleza mila na desturi za jamii ya Wasukuma. Naye mdau wa utamaduni kutoka Kenya, Dominic Mkami alisema amefika Shinyanga kumuunga mkono Peter Lugumi maarufu ‘Mr Black’ kwa kazi yake ya kutunza utamaduni wa Msukuma.

Post a Comment