DC Ilala: Viongozi wanaodhulumu haki za wananchi wanaitukanisha Serikali
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema viongozi wanaoshindwa kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na wanaohusika na vitendo vya kudhulumu mashamba na viwanja wanaitukanisha Serikali.
Akizungumza baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wakati wa mkutano uliofanyika katika Kata ya Zingiziwa, Mtaa wa Nzasa, Mpogolo alieleza kuwa viongozi hupimwa kwa maadili na utendaji wao, na kwamba pale kiongozi anapolalamikiwa mara kwa mara na wananchi wake, ni ishara ya uwepo wa dosari kubwa katika utoaji wa huduma.
Aliongeza kuwa wananchi wengi wanaopaza sauti zao wanapitia changamoto zinazohusu maisha yao ya kila siku ya kutafuta kujikwamua kiuchumi kupitia kumiliki viwanja, kujenga makazi, na kuhudumia familia zao, jambo linalowapasa viongozi kuwaonesha huruma na kuwapatia huduma stahiki.
Alisema kuwa viongozi wa ngazi za chini wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo huathiri taswira ya Serikali nzima kwa sababu lawama hupanda hadi kwa viongozi wa juu ikiwemo kwa Rais, ambaye amekuwa akiongoza nchi kwa falsafa ya 4Rs na kaulimbiu ya Kazi na Utu inayowataka viongozi kuzingatia uadilifu na utu katika kuwahudumia wananchi.
Mpogolo aliwapongeza baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kazi nzuri huku akiwataka wale wenye mapungufu kuboresha utoaji huduma kwa kukumbuka kuwa walichaguliwa kuwatumikia wananchi na kwamba baada ya muda watarudi kwa wananchi haohao.
Alisisitiza kuwa hakuna jambo linalobaki kwenye kumbukumbu za wananchi kama huduma njema na kwamba viongozi wanaowatumikia watu kwa haki hukumbukwa kwa mema hata baada ya kuondoka madarakani.
Kufuatia malalamiko yaliyotolewa kuhusu mgogoro wa mashamba na viwanja katika Mtaa wa Somero, Mpogolo alitangaza kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Hassan Ramadhani, ambaye ametajwa mara kwa mara katika malalamiko hayo, atawekwa pembeni kwa muda ili kupisha uchunguzi huru utakaofanywa na wataalamu wa ardhi, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wanasheria wa jiji.

Post a Comment