DC MPOGOLO ATAKA USAFI KUWA SEHEMU YA KILA SIKU YA MAISHA
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, ameongoza zoezi la usafi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, huku akiwataka wananchi kufanya usafi kuwa sehemu ya utamaduni wao wa kila siku ili kulinda afya na mazingira yao.
Zoezi hilo limefanyika , Agosti 22, 2026, katika Mtaa wa Lumumba, Mnazi Mmoja, Kamata, Fukwe za Dengue na maeneo mengine ya katikati ya jiji, likiwaleta pamoja wananchi na wadau mbalimbali wa usafi katika kukusanya taka na kusafisha maeneo ya umma.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Mpogolo amewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo na badala yake kuhakikisha wanatunza mazingira yao kila siku badala ya kusubiri siku maalum au kufanya usafi mara moja kwa wiki pekee.
Alisema kuwa usafi unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi ili kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwa safi, salama na lenye mazingira bora yanayovutia.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za serikali katika kutunza usafi wa mazingira, akieleza wazi kuwa jukumu la kulifanya jiji kuwa safi sio la serikali pekee bali ni la kila mkaazi.
Zoezi hilo ni miongoni mwa mikakati endelevu inayochukuliwa na uongozi wa Jiji la Dar es Salaam katika kuimarisha usafi wa mazingira na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu.

Post a Comment