Benki ya Dunia Yafungua Milango Kufadhili Awamu ya Pili ya Maboresho Bandari ya Dar es Salaam
Benki ya Dunia imesifu uhusiano thabiti uliopo kati yake na Tanzania huku ikitoa sifa za kipekee kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kusimamia kwa ufanisi mkubwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia mpango wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP).
Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kikao kifupi na wajumbe wa TPA, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshuhulikia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, alieleza kuwa mabadiliko makubwa na ongezeko la shehena inayohudumiwa bandarini hapo ni ushahidi wa wazi wa mafanikio ya ushirikiano huo, akisisitiza umuhimu wa bandari hiyo katika kuhudumia nchi sita za jirani zisizo na bandari.
Kutokana na ufanisi huo, Dkt. Diop ameahidi kuendelea kuishawishi benki hiyo ili iunge mkono awamu ya pili ya maboresho ambayo yatajikita katika ujenzi wa gati mpya na eneo maalumu la kuegeshea magari, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, alieleza kuwa mafanikio haya yaliyofikiwa kupitia mkopo wa Dola za Marekani milioni 421 kutoka Benki ya Dunia na mchango wa Serikali ya Tanzania wa Dola milioni 64 yameiwezesha bandari hiyo kuongeza uwezo wake wa kupitisha shehena kutoka tani milioni 14 za mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani milioni 33 hivi sasa, jambo lililoifanya iteke soko la nchi zinazozunguka Tanzania ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, na Zambia.
Maboresho haya yanatajwa kuwa chachu kubwa kwa wawekezaji wakubwa na wadogo kujenga viwanda, huku yakiwapa vijana fursa za kujiajiri kupitia biashara na kilimo kwa kuuza mazao yao nje ya nchi kwa urahisi kupitia lango kuu la bahari.

Post a Comment