Balozi Saidi Yakubu ateta Hifadhi ya Magofu ya Kilwa ni urithi



BALOZI wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Saidi Yakubu amesema Hifadhi ya Magofu ya Kilwa ni urithi mkubwa unaopaswa kuenziwa, kulindwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. 

Balozi Yakubu alisema hayo alipofanya ziara katika Hifadhi ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara mkoani Lindi ambayo imetambuliwa na Unesco kuwa Urithi wa Dunia. 

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kutembelea maeneo ya urithi wa dunia nchini, kujionea hali ya uhifadhi wake na kuimarisha ushirikiano na Unesco na wadau wengine wa kimataifa.

 “Hifadhi ya Magofu ya Kilwa ni urithi mkubwa unaopaswa kuenziwa, kulindwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. Tunapaswa pia kutambua na kuthamini mchango wa serikali ya Marekani, World Monuments Fund na serikali ya Ufaransa ambao kwa nyakati tofauti wameunga mkono juhudi za Tanzania katika kuhifadhi na kuyatunza magofu haya,” alisema.

Akiwa Kilwa, Balozi Yakubu alijionea historia adhimu iliyobebwa na magofu hayo, ikiwemo ushahidi wa ustaarabu, biashara na mahusiano ya Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali za dunia yaliyodumu kwa karne nyingi. 

Alisisitiza kuwa Kilwa si urithi wa Tanzania pekee, bali ni sehemu muhimu ya simulizi ya historia ya Afrika na dunia. 

Aidha, aliipongeza serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa juhudi za kulinda eneo hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuvutia ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi, tafiti, miundombinu na utalii endelevu.

 Balozi Yakubu pia amehimiza kuongeza ubunifu wa mazao ya utalii katika Kilwa, yakiunganisha historia ya magofu, utamaduni wa jamii, utalii wa baharini, mikoko na vivutio vingine vya ukanda huo. 

Alisema uhifadhi wa urithi unapaswa kwenda sambamba na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya urithi. “Kilwa ina historia yenye uwezo mkubwa wa kuitangaza Tanzania duniani. 

Jukumu letu ni kuhakikisha tunailinda, tunaitangaza na tunaifanya historia hii iwe chanzo cha elimu, utalii na maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Balozi Yakubu.


No comments