SAYANSI KUPEWA NAFASI KUTHIBITISHA TIBA ASILIA


 Serikali imeongeza msukumo wa kuunganisha tiba asilia na tiba za kisasa kwa kuwataka wanasayansi na wataalamu wa afya nchini kutumia mbinu za kisayansi kuthibitisha ufanisi wa maarifa ya tiba za jadi zinazotumiwa na wananchi kabla ya kuziingiza katika mfumo rasmi wa huduma za afya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema tiba asilia zinapaswa kufanyiwa utafiti wa kina, majaribio ya kitabibu (clinical trials) na tathmini za kitaalamu ili kubaini usalama, ufanisi, dozi sahihi na matumizi yake kwa makundi mbalimbali ya wagonjwa.

Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali si kuondoa au kudharau tiba asilia, bali kuiboresha na kuipa nguvu kupitia sayansi ili iweze kutumika kwa usalama ndani ya mfumo wa afya wa kisasa. Alisema ni wajibu wa sayansi kuchunguza, kuthibitisha na kubaini ukweli wa madai yote ya tiba, iwe ya kisasa au ya jadi, kupitia mbinu madhubuti za utafiti.

“Tunapochunguza madai ya ufanisi, iwe kutoka tiba asilia au nyinginezo, jukumu la sayansi liko wazi, kupima, kuthibitisha na kuanzisha ukweli kupitia mbinu madhubuti,” alisema. Prof. Mkenda. Alisisitiza kuwa lengo si kukataa tiba asilia, bali kuiinua kupitia sayansi na kuhakikisha matumizi yake salama ndani ya huduma za afya za kisasa.

No comments