Rais Abdel Fattah El-Sisi kuwasili kwa ziara ya kitaifa leo
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Abdel Fattah El-Sisi, anatarajiwa kuwasili nchini leo tarehe 18 Julai, 2026 kwa ajili ya kufanya ziara ya kitaifa ambayo inalenga kuendeleza uhusiano mwema kati ya mataifa haya mawili.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Rais El-Sisi atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo viongozi hao watajadili namna ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria uliopo na kupanua wigo wa ushirikiano katika sekta muhimu za maendeleo ikiwemo biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, maji, afya, elimu, na miundombinu.
Katika kuongeza chachu ya ushirikiano wa kiuchumi, viongozi hao watashiriki katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Misri litakalowakutanisha wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka pande zote mbili ili kujadili na kutathmini fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji.
Hatua hii inakuja kufuatia ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo mbili ambao umekuwa ukijikita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, mafunzo ya wataalamu, na ubadilishanaji wa uzoefu.
Ziara hii inatazamiwa kutoa msukumo mpya na kuimarisha ushirikiano wenye tija ambao utawanufaisha wananchi wa Tanzania na Misri kwa ujumla.

Post a Comment