KLABU ZISIFANYE MAKOSA DIRISHA LA USAJILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi mbio za kuelekea msimu mpya wa mashindano wa 2026/2027 kwa kufungua dirisha kubwa la usajili wa wachezaji kuanzia Julai 6 hadi Agosti 15 mwaka huu saa 5:59 usiku.
Hatua hii inahusisha klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League, Ligi Kuu ya Wanawake pamoja na Ligi Kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20.
TFF imetoa msisitizo wa kipekee kwa klabu zote kukamilisha taratibu zote za usajili na uhamisho wa wachezaji ndani ya muda uliopangwa kupitia mfumo wa kidijitali wa FIFA Connect, ikibainishwa wazi kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza utakaotolewa baada ya tarehe hiyo ya ukomo kupita.
Katika msimu huu, uchambuzi wa kina unaonyesha kuwa usajili hautakuwa wa kimazoea kwani umegubikwa na mkazo mkubwa wa kisheria na kimkakati kutoka kwa uongozi wa juu wa shirikisho.
Rais wa TFF, Wallace Karia, ameweka wazi kuwa msimu huu umeandaliwa kwa jicho la kipekee ili kuhakikisha kalenda ya mashindano ya ndani inaendana kikamilifu na maandalizi ya timu za taifa, hasa ikizingatiwa kuwa nchi inajiandaa na mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Ratiba hii iliyobana inalazimisha klabu kuwa makini katika kuwasilisha nyaraka sahihi na zilizokamilika mapema ili kuepuka ucheleweshaji wa michakato inayoweza kuingia kwenye mzozo na Idara ya Mashindano, ambayo imejipanga kutoa msaada wa haraka kwa klabu zitakazokutana na changamoto za kimfumo.
Eneo linalotarajiwa kuleta mtikisiko mkubwa kwa klabu zenye ukwasi wa kifedha ni utekelezaji wa Kanuni ya 62 (4) ya Ligi Kuu Tanzania inayohusu sifa za wachezaji wa kigeni.
TFF imetangaza kuifanyia kazi kanuni hii kwa dhati kwa kutilia mkazo kuwa wachezaji wa kigeni watakaoruhusiwa kusajiliwa ni wale tu wanaocheza katika timu za taifa za nchi zao.
Hatua hii inalenga kuinua kiwango cha ushindani wa ligi na kuhakikisha wachezaji wanaokuja nchini wana tija ya moja kwa moja.
Ingawa huko nyuma utekelezaji wake uliingia changamoto kwa kuruhusu mchezaji aliyetoka klabu inayoshiriki ligi kuu ya nchi yoyote kusajiliwa hata kama hachezi timu ya taifa, msimu huu mkazo mkubwa utakuwa kwenye vigezo vya timu ya taifa, hatua inayolazimisha maskauti na viongozi wa klabu kufanya tathmini ya kina kabla ya kuingia mikataba.
Kutokana na mabadiliko hayo, mchakato wa uwasilishaji wa nyaraka kupitia njia tatu za mfumo—iwe ni usajili wa mara ya kwanza, uendelezaji wa mkataba, au uhamisho wa jumla na wa mkopo—utahitaji umakini wa hali ya juu.
Klabu zinatakiwa kuwasilisha mikataba ya ajira, barua za uhamisho au kuachwa huru, vyeti vya afya, picha na nakala za malipo kwa usahihi.
Kwa wachezaji wa kigeni, mahitaji yatakuwa makali zaidi yakihusisha Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini.
Mkakati huu wa TFF sio tu kwamba unalinda hadhi ya soka la Tanzania, bali unazilazimisha klabu kujenga mifumo ya kiutawala inayofanya kazi kitaalamu ili kuepuka adhabu na migogoro ya kisheria na wachezaji au klabu nyingine ndani na nje ya nchi.
Post a Comment