SIMANZI: Mkongwe wa maigizo Mzee Onyango atangulia mbele ya haki, tasnia na umma walia na pengo lake


Tasnia ya sanaa na utamaduni nchini imegubikwa na wingu zito la majonzi kufuatia kifo cha mwigizaji mkongwe na fundi wa sauti, Issa Joseph, aliyefahamika zaidi kwa jina la sanaa la Mzee Onyango. 

Mkongwe huyo aliyekuwa na umri wa miaka 70, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa akipatiwa matibabu. 

Taarifa za kuondoka kwa gwiji huyo zimeleta mshtuko mkubwa kwa mashabiki wa sanaa wa vizazi tofauti, kutokana na mchango wake uliotukuka ulioanza tangu enzi za utangazaji wa redio hadi kuingia kwa filamu za kisasa.

Mtoto wa marehemu, Joseph Issa, amethibitisha msiba huo akieleza kuwa baba yake alifikwa na umauti majira ya saa saba usiku baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu kwa muda mrefu. 

Akizungumza kwa masikitiko, Joseph amebainisha kuwa marehemu alikuwa akipata nafuu mara kwa mara na kuendelea na majukumu yake, lakini safari hii ugonjwa huo ulijirudia kwa nguvu kubwa zaidi na kusababisha kifo chake ghafla kabla ya madaktari hawajafanikiwa kuokoa maisha yake. 

Taarifa hizo zimeungwa mkono na msanii mwenzake wa karibu, Seif Mbembe, aliyeelezea msiba huo kama pigo kubwa kwa jamii ya wasanii kutokana na nafasi ya kipekee aliyokuwa nayo marehemu katika tasnia.

Kumbukumbu za Mzee Onyango zimebaki imara mioyoni mwa Watanzania wengi, hususan wale waliokulia katika enzi za dhahabu za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Mkongwe huyo alijizolea umaarufu mkubwa kupitia vipindi vya maigizo ya redio vilivyotikisa nchi ikiwemo michezo maarufu kama 'Mahoka', ambapo uwezo wake wa kubadilisha sauti, ucheshi na uwasilishaji wa ujumbe wenye maadili ulimfanya kuwa kipenzi cha wasikilizaji wengi. 

Baadaye alihamishia kipaji chake kwenye skrini ya runinga na filamu, aking'ara katika kazi zilizopendwa sana kama vile 'Babu The Perfect Man', 'Ripoti', na 'Kimbembe', ambazo zilithibitisha ukomavu wake katika uigizaji.

Mbali na mchango wake mkubwa katika tasnia ya burudani, Mzee Onyango alikuwa mtu mwenye historia ya kipekee ya kizalendo, ambapo katika uhai wake aliwahi kuweka wazi kuwa alikuwa mmoja wa mashujaa waliopigana katika Vita vya Kagera vya mwaka 1978 na 1979 akihudumu kama mwendeshaji wa mitambo ya mawasiliano. 

Uzoefu huo wa maisha ya kijeshi na ukongwe katika sanaa ulimfanya kuwa mlezi, mshauri na nguzo muhimu kwa wasanii chipukizi waliokuwa wakitafuta dira ya mafanikio katika tasnia ya maigizo nchini Tanzania.

Kwa sasa, viongozi wa mashirikisho ya sanaa, ndugu, jamaa na wasanii wenzake wameanza kukusanyika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Kawe Triple Seven jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa mkono wa heri na faraja kwa familia. 

No comments