KAMA HUNA UWEZO USIOMBE KAZI ILALA - DC MPOGOLO
Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka wakandarasi wenye nia ya kuja kuomba kazi katika Wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hizo.
Ametoa angalizo hilo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kimanga-Mazda yenye urefu wa mita 400 iliyojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.7 fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mhe. Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 14 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutengeneza na kuboresha barabara ndani ya Jiji hilo hali ambayo itafanya wakandarasi wengi kuvutiwa kuja kuomba mkataba wa kufanya kazi za ujenzi wa barabara.
"Najua kwa kiasi hiki cha fedha wakandarasi wengi watatamani kuja kuomba kazi hapa kwetu Ilala, ila hatutawavumilia wakandarasi wasiokuwa na uwezo, kama huna uwezo usije kuomba kazi hapa." Alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha katika miradi mbalimbali ya Elimu, Afya na miundombinu ya barabara.
Barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi mzawa kampuni ya Osaka Construction Ltd ni kiungo muhimu kati ya Wilaya ya Ilala na Ubungo ambayo hapo awali ilikuwa na changamoto ya kupitika hasa nyakati za mvua.
Post a Comment