POLISI WAFICHUA MPANGO WA UHALIFU JULAI 7
Jeshi la Polisi
limetoa onyo kali kwa watu wote wanaohamasisha na kupanga kutekeleza vitendo
vya uvunjifu wa amani na uhalifu nchini, wakiwemo wale wanaochochea kufanyika
kwa maandamano mnamo tarehe 7 Julai mwaka huu.
Onyo hilo limetolewa
kufuatia kuwepo kwa maswali mengi kutoka kwa baadhi ya wananchi hivi karibuni,
wakitaka kujua jinsi jeshi hilo linavyofuatilia na kushughulikia uhamasishaji
huo wa uvunjifu wa amani unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu kupitia
majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
Kupitia taarifa yake,
Jeshi la Polisi limesema linafuatilia kwa karibu sana shughuli hizo zote
kupitia mifumo yake mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, ambapo
imegundulika kuwa watu hao wameacha ajenda ya awali ya maandamano
yasiyozingatia sheria na sasa wanahamasishana kufanya vitendo vizito vya
kihalifu.
Miongoni mwa vitendo
vya hatari vinavyohamasishwa ni pamoja na kufunga barabara, kuchoma moto shule
kwa lengo la kusababisha taharuki kwa wazazi na walezi, kushambulia wananchi,
kukata watu vichwa na kuua, pamoja na kuharibu mali za umma na za binafsi.
Aidha, watu hao
wamediriki kwenda mbali zaidi kwa kuchocheana kupitia mitandao hiyo kuvamia
askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuwapora silaha kwa ajili ya kwenda
kuzitumia kutekeleza uhalifu wanaoupanga.
Jeshi la Polisi
limesisitiza kuwa uhamasishaji huo wa jinai unaofanyika chini ya kivuli cha
kile wanachokiita haki ya kufanya maandamano ya amani haukubaliki hata kidogo,
kwani ni kinyume kabisa na sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria,
mikataba ya kikanda na kimataifa, na unahatarisha usalama wa Taifa.
Jeshi hilo
limefafanua kuwa hakuna haki yoyote inayomruhusu mtu kuhamasisha uhalifu
unaokusudia kuhatarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao, au unaokiuka
haki za wengine kwa kuwajengea hofu kila siku na kuwanyima uhuru wao wa kufanya
shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.
Kwa sababu hiyo, Jeshi
hilo limesema hatua stahiki za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya
wahusika wote, na jeshi linaendelea kuwafuatilia kwa karibu sana kwa mujibu wa
sheria za nchi.
Jeshi la Polisi
limetoa wito kwa wananchi wote nchini kuungana kwa pamoja katika kushirikiana
kukataa na kupinga kwa nguvu zote vitendo hivyo vya kihalifu vinavyolenga
kuhatarisha maisha ya wananchi, mali zao, mali za umma, pamoja na amani ya
nchi.
Vilevile, limetoa
ushauri kwa mtu yeyote anayepokea ujumbe unaohamasisha uhalifu wa aina hiyo
kutousambaza kabisa, bali kuufuta mara moja na kutoa taarifa kwa vyombo husika
ili hatua zichukuliwe.
Jeshi
limewahakikishia wananchi wote kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa
shwari, yenye amani, utulivu na usalama kamili, kwani mambo hayo yatalindwa na
kudumishwa kwa ushirikiano wa karibu sana kati ya Jeshi la Polisi pamoja na
vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama.

Post a Comment