Mfahamu Elieneza Nsanganzelu na Safari ya Serengeti Boys Kuelekea Qatar


Jina lake limegeuka kuwa maarufu ghafla baada ya mbinu zake kuwa habari ya mjini kote nchini. Alianza kimyakimya kama maji ya mtungi, lakini akaibuka kwa kishindo kama dhoruba ya uwanjani inayozwika. Sasa wapenzi wa soka wanauliza kwa mshangao, huyu kijana anatoka wapi na mbinu hizi anazitoa wapi? 

Ndani ya dakika tisini za mchezo, saini yake inaonekana kwenye kila pasi na kila bao linalofungwa uwanjani. Yeye si kocha wa kawaida tu, bali ni mchawi wa ubao wa mbinu ambaye ametoa hofu miili ya wachezaji na kuweka roho ya ubingwa. Kila mtu sasa anatusalimia baada ya yeye kuipa pumzi ya ushindi timu ya Taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, katika michuano ya Mataifa ya Afrika ya AFCON kule nchini Morocco.

Huyo ni Elieneza Nsanganzelu, kijana wa Kitanzania mzaliwa wa Endasak wilayani Hanang mkoani Manyara, ambaye wazazi wake wote ni Wanyisanzu wenyeji wa Mkoa wa Singida. 

Jina lake sasa limeandikwa kwa wino wa dhahabu usiofutika mioyoni mwa Watanzania. Kutokana na malezi aliyoyapata nyumbani, angeweza kuwa mtumishi wa Mungu kwa sababu baba yake ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mbulu, Nicolaus Nsanganzelu, lakini alichagua kufuata njia ya ndoto zake ambayo ni soka. 

Ni fundi aliyebadili upepo kabisa baada ya kukabidhiwa vijana hawa na kuwapa mbinu za ushindi ambapo walitawala uwanjani, na kila aliyekutana na kikosi chake aliondoka akilia huku Watanzania wakijivunia uwepo wake. Pamoja na kuwa hapo awali hakuna aliyemjua sana wala kutarajia makubwa, amethibitisha kuwa uwezo hauji kwa jina kubwa bali kwa vitendo, na kuipa Tanzania heshima katikati ya mataifa vigogo.




Safari yake ya maisha ilianza kama Mwalimu wa Shule ya Sekondari Ndala iliyopo mkoani Shinyanga, lakini alifanya kazi hiyo kwa muda mfupi tu kutokana na mapenzi yake makubwa kwenye soka yanayomfanya asitulie darasani.

 Elieneza ambaye kwa sasa anahudumu kama Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, amehudumu karibu timu zote za umri za Taifa ikiwemo Serengeti Girls. Kabla hajaanza kufundisha timu hizo, alikuwa kocha wa viungo wa timu ya wakubwa ya Taifa Stars kuanzia mwaka 2020. Huko nyuma pia alikuwa kocha katika Kituo cha Michezo cha Jakaya Kikwete cha Kidongo Chekundu Mnazimmoja jijini Dar es Salaam. 

Kadhalika amewahi kuwa kocha wa viungo wa klabu ya Yanga wakati timu hiyo ikifundishwa na Cedric Kaze, na pia mwaka 2025 alikuwa kocha mkuu wa Simba Queens ambapo hakudumu kutokana na kuitwa kulitumikia taifa kujiandaa na Serengeti Boys. Katika upande wa elimu, alisoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku akiwekeza sana kwenye kozi za michezo na ukocha wa kisasa katika nchi za Ujerumani na Afrika Kusini.

Kwa miaka mingi soka la Tanzania liliishi katika vivuli vya wababe wa Afrika, lakini kwenye jukwaa kubwa zaidi la vijana barani, Serengeti Boys wameacha simulizi ya milele katika michuano hiyo iliyoanza Mei 13 hadi Juni 2 mwaka huu. 





Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa, Serengeti Boys iling'atua timu kutoka mataifa yanayoaminika kuwa vigogo chini ya mikono ya Elieneza. Walifungua ukurasa kwa kuzifunga Angola mabao matatu kwa sifuri, wakaipiga Msumbiji mabao matatu kwa sifuri, kabla ya kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Mali kwa mabao mawili kwa moja katika hatua ya makundi. 

Kipigo hicho hakikuwakatisha tamaa kwani katika hatua ya robo fainali, waliiondosha Algeria kwa penalti nne kwa tatu baada ya sare ya mabao matatu kwa matatu. Katika nusu fainali walisonga mbele kwa kuwatoa Misri kwa penalti nne kwa tatu kufuatia suluhu ya bila kufungana, hatua iliyowapa tiketi ya kutinga Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026.

Ushahidi wa kazi nzuri ya mbinu za Elieneza ulionekana wazi baada ya Serengeti Boys kufanikiwa kutoa wachezaji wanne katika kikosi bora cha mashindano hayo barani Afrika, idadi inayolingana na mabingwa Senegal. 

Wachezaji hao waliong'ara ni mshambuliaji Razaki Mbelegendi, kiungo na mfungaji bora wa mashindano Dismas Athanas, kiungo wa ulinzi ambaye pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano Issa Chole, pamoja na beki wa kati Hussein Mbegu. 

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa timu ya wanaume kufuzu Kombe la Dunia, na ni mara ya tatu kwa ujumla katika soka baada ya Serengeti Girls kufuzu mwaka 2022 na Tanzanite Queens kufuzu mwaka huu, ambapo timu zote hizi zilizofanya maajabu zinafundishwa na makocha wazawa akianza Bakari Shime na sasa Elieneza Nsanganzelu.

Mwenyewe Elieneza anasisitiza kuwa hakuna muujiza wowote katika soka bali siri kubwa ni uwezekano, kuweka wachezaji pamoja, mafunzo ya mfululizo, na kushindana mara kwa mara. 

Amewataka watoto wote kuamini katika ndoto zao na kufanya mazoezi kwa bidii. Anasema somo kubwa alilowajaza vijana wake ni kwamba fikra zao lazima ziwe juu zaidi ya wapinzani wao, kwani timu nyingi hupoteza mechi kisaikolojia kwa kuogopa majina ya nchi kubwa kabla hata hawajaingia uwanjani. 

Anamalizia kwa kusema kuwa kile wanachokifanya ni kitu sahihi na wataendelea nacho, huku akitoa wito kuwa mafanikio haya yakachochee uwekezaji mkubwa zaidi katika akademi za michezo, elimu ya ukocha, skauti, na mashindano ya vijana ili kukuza vipaji vipya katika njia inayofaa.

No comments