Bajeti ya Shilingi Trilioni 62.33 Kuzindua Rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050



Serikali imewasilisha mapendekezo ya kihistoria ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikitangaza bajeti ya Shilingi trilioni 62.33.

Bajeti hii inatajwa kuwa ya kipekee kwani ndiyo inayozindua rasmi utekelezaji wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27 - 2030/31).

Akiwasilisha hotuba hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amebainisha kuwa bajeti ya mwaka huu imeshuhudia ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita. 

Ongezeko hili linaashiria upanuzi mkubwa wa shughuli za kiuchumi na azma ya serikali ya kuongeza uwekezaji wa kimkakati.

Katika sura hiyo mpya, serikali inakadiria kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya Shilingi trilioni 46.79, ambapo mapato ya kodi pekee yanatarajiwa kuwa Shilingi trilioni 36.99. 

Hatua hii inalenga kuifikisha nchi katika uhuru kamili wa kibajeti (fiscal sovereignty) , ambapo takriban robo tatu ya bajeti nzima sasa itagharamiwa na rasilimali za ndani badala ya kutegemea misaada ya nje.

"Hatua hizi zinalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji, na kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kujitegemea katika ugharamiaji wa sehemu kubwa ya Bajeti ya Serikali," alisema Balozi Omar. Serikali imeweka malengo ya kukuza Pato Halisi la Taifa kwa asilimia 6.3 huku ikidhibiti kwa karibu mfumuko wa bei ubaki katika kiwango cha wastani wa asilimia 3.0 hadi 5.0.

No comments