WANASAYANSI WAZUNGUMZIA MPIRA WA TRIONDA KWA WAPENDA MASHUTI YA MBALI
Na
Mwandishi Maalumu
Wakati homa ya Kombe la Dunia
ikizidi kupanda, mjadala mzito umehamia kwenye maabara za sayansi ya michezo,
huku wanasayansi wakitupa onyo mapema kwa wapiga mashuti ya mbali kujiandaa na
mabadiliko makubwa ya mpira rasmi wa mashindano hayo unaojulikana kama Trionda.
Mpira huo uliotengenezwa na kampuni
ya Adidas, umeingia kwenye historia ya Kombe la Dunia kuwa mpira wa kwanza
kuwahi kutengenezwa kwa kutumia vipande vinne tu (4 panels).
Idadi hiyo ndogo ya vipande ilizua
hofu ya mapema kuwa mpira huo ungekuwa mnyororo sana (smooth profile) na kuanza
"kuyumba na kupaa" hewani kama ule mpira wa hovyo wa Jabulani
uliosababisha vilio kwa makipa kwenye Kombe la Dunia la mwaka 2010 nchini
Afrika Kusini.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya
usugu wa hewa (aerodynamics) wamebaini kuwa 'Trionda' una tatizo la tofauti
kabisa: Mashuti ya mbali yatakuwa yanapungua kasi na kuishia njiani!
Wanasayansi hao hawatilii shaka ubora wa mpira mpya wa Kombe la Dunia, Trionda, bali wanahoji uwezo wake
wa kusafiri umbali mrefu unapovurumushwa kwa nguvu kubwa. Mashaka yao makuu
yamegawanyika katika maeneo matatu:
·
Kupunguza Kasi na Kuishia Njiani: Ngozi ya kwaruza na
mifereji mirefu ya mpira huo husababisha upinzani mkubwa wa upepo (drag). Shuti kali la mbali
litapoteza nguvu haraka na kuanguka hadi mita 10 mapema kuliko mipira ya miaka ya nyuma.
·
Mtihani kwa Wapigaji Mashuti ya Nguvu: Wachezaji
wanaotegemea mashuti makali ya mbali na pasi ndefu watajikuta wakifeli kupata
kasi na umbali waliozoea, jambo litakalowalazimu kubadili mbinu zao za upigaji
uwanjani ili kufidia mita hizo 10 zinazopotea.
·
Kupinda Zaidi Hewani (Extreme Spin): Muundo wa kwaruza unawaongezea
faida wapiga free-kick
mafundi kwani mpira utapinda kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida, hatua
itakayowapa wakati mgumu magolikipa kuotea mwelekeo wake wa mwisho.
Siri
ya Mistari na Ngozi ya Trionda
Ili kufidia uhaba wa mishono (seams)
ambao ungeufanya mpira kuwa mnyororo mno, Adidas waliongeza mifereji mirefu
(deep grooves) kwenye kila kipande, pamoja na kuuweka mtindo wa ngozi ya
kwaruza (rough outer texture).
Mwanasayansi wa fizikia kutoka Chuo
Kikuu cha Puget Sound, Dk. John Eric Goff, ameeleza kuwa uamuzi huo wa Adidas
umebadilisha tabia ya msuguano wa hewa (drag crisis), jambo ambalo litawaumiza
vichwa washambuliaji wanaopenda kupiga mashuti ya mbali au mabeki wanaopiga
pasi ndefu.
“Kwa lugha rahisi, maana yake ni
kwamba shuti kali la mbali litakuwa linapoteza nguvu na umbali hewani. Kwenye
majaribio yetu ya kompyuta, tofauti hiyo si kubwa sana, lakini inatosha kabisa
kwa wachezaji kugundua kuwa mashuti yao yanaangukia mita chache kabla ya pale
walipokusudia,” alieleza Dk. Goff.
Mizania
ya Kitaalamu: Trionda vs Mipira ya Zamani
Wanasayansi walifanya majaribio hayo
kwa kuingiza mpira huo kwenye mtambo maalum wa upepo (wind tunnel) ili kupima
kasi ambapo mpira huanza kupoteza mwelekeo (drag crisis point). Habari njema ni
kwamba Trionda utakuwa mpira imara na unaotabirika kuliko Jabulani.
Hapa kuna ulinganifu wa kasi ambayo
mpira huanza kupoteza utulivu (Drag Crisis Speed):
|
Jina la Mpira |
Mwaka wa Kombe la Dunia |
Kasi ya Kupoteza Utulivu (Km/h) |
Hali yake Uwanjani |
|
Jabulani |
2010 (Afrika Kusini) |
Km/h 79 – 97 |
Haubadiriki, ulikuwa unacheza na kuyumba hewani ghafla. |
|
Brazuka |
2014 (Brazil) |
Km/h 50 – 65 |
Imara na wa kawaida. |
|
Telstar 18 |
2018 (Urusi) |
Km/h 50 – 65 |
Imara na wa kawaida. |
|
Al Rihla |
2022 (Qatar) |
Km/h 50 – 65 |
Imara na wa kawaida. |
|
Trionda |
Mwaka Huu |
Km/h 43 pekee |
Hauyumbi kabisa, lakini unapunguza umbali ukiwa hewani. |
Kwanini Jabulani Ikishindikana na Trionda ni Salama?
Tangu mwaka 1970, Adidas wamekuwa wakileta mipira mipya
kwenye kila fainali za Kombe la Dunia, lakini mabadiliko madogo tu ya muundo
hugusa moja kwa moja burudani ya uwanjani.
Dk. Goff na timu yake waliiweka Trionda kwenye mtambo wa upepo (wind tunnel)
kupima uwezo wake wa kuhimili hewa na kuingiza data hizo kwenye kompyuta.
Siri kubwa ya mpira uliotulia uwanjani ipo kwenye hatua
inayoitwa kitaalamu kama 'drag
crisis'. Mpira ukiwa hewani, safu nyembamba ya hewa hunaswa pembezoni mwa
ngozi yake na kuusaidia kusafiri mbali. Mpira ukiwa mnyororo kupitiliza kama
Jabulani, hufikia hatua hii ukiwa tayari kwenye kasi ya mchezo, na kusababisha
mabadiliko ya ghafla ya mwelekeo (erratic flight).
Trionda haina ugonjwa huo wa Jabulani. Inafikia hatua
yake ya utulivu kwenye kasi ndogo ya kilomita 43 tu kwa saa, tofauti kabisa na
Jabulani iliyokuwa ikiyumba ikifikia kasi ya kilomita 79 hadi 97 kwa saa. Hii
ina maana Trionda utakuwa mpira unaotabirika na mtulivu sana kwenye krosi,
kona, na mipira ya adhabu.
Mita 10 za Kupotea: Habari Njema kwa Magolikipa
Hata hivyo, utulivu huo una gharama yake. Ripoti hiyo
inafichua kuwa pindi Trionda unapopigwa kwa nguvu kubwa ya mbali, unakutana na
upinzani mkubwa wa upepo kuliko mpira wowote uliowahi kutumika katika kipindi cha
miaka 20 iliyopita.
Kwenye vipimo vya kimaabara, shuti linalopigwa kwa kasi
ya mita 35 kwa sekunde, mpira wa
Trionda utaanguka umbali wa mita 10 fupi ukilinganishwa na mipira ya Al Rihla (2022) au Brazuka (2014).
Hili ni dongo gizani kwa wapiga
mashuti ya mbali, lakini ni sherehe kwa magolikipa watakaopata sekunde chache
za ziada kujipanga.
Mwisho, wataalamu wametoa angalizo lingine: ngozi hiyo
ya kwaruza inaweza kuwasaidia wachezaji mafundi kuuzungusha mpira hewani (spin) kwa kiwango kikubwa
zaidi. Hii ina maana mashuti yanaweza yasiende mbali sana, lakini yale
yatakayofika golini yatapinda kwa pembe kali, jambo ambalo linaweza kurudisha
ugumu huo huo kwa walinda milango.
Post a Comment