Serikali ya Zanzibar Yaunga Mkono Ripoti ya Jaji Chande, Yaonya Siasa za Vurugu kwa Vijana



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)imesema inaunga mkono ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwataka wanasiasa kuacha kuwashawishi vijana kujiingiza katika vurugu za kisiasa zinazohatarisha maisha yao na usalama wa taifa. 

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma, wakati akitoa maoni ya serikali kuhusu ripoti hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman ambayo tayari imewasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Juma alibainisha kuwa tume imefanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya vurugu yaliyojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, na Arusha, na kubaini kuwa baadhi ya wanasiasa walitumia ushawishi wao kuwahusisha vijana katika vurugu hizo kwa lengo la kuvuruga mchakato wa uchaguzi, jambo lililosababisha uharibifu wa mali na kupotea kwa maisha ya baadhi ya wananchi.

Waziri Juma aliwaomba wanasiasa kufanya siasa za kujenga nchi na kuhubiri uzalendo badala ya kuwashawishi vijana kuingia katika vurugu ambazo athari zake ni kubwa kwa taifa na kwa maisha yao binafsi, huku akisisitiza kuwa nguvu kazi hiyo inapaswa kuelekezwa katika fursa za uzalishaji mali na ujasiriamali. 

Alisema changamoto ya ukosefu wa ajira isitumiwe kama kigezo cha kuwatumia vijana kwa maslahi ya kisiasa, bali sekta binafsi ipewe nafasi ya kuwasaidia kujiajiri na kujitegemea kiuchumi ili kuimarisha ustawi wao. Aidha, aliwasihi vijana wenyewe kuwa macho na kuepuka kushawishiwa kujiingiza katika vurugu, na badala yake wazingatie uzalendo, kuheshimu sheria za nchi, na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya kitaifa.

Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo alieleza kuwa serikali imejifunza kutokana na matukio ya nyuma na imekuwa ikiendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kulinda amani na utulivu wa nchi, jambo lililopelekea uchaguzi mkuu uliopita visiwani humo kufanyika kwa amani kubwa na kupongezwa na waangalizi wa ndani na nje ya nchi. 

Alisema vurugu zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu zinapaswa kuwa fundisho la umuhimu wa vijana kuwa wazalendo wa kweli na kujiepusha na ushawishi wa wanasiasa wenye tamaa ya madaraka ambao wako tayari kuhatarisha amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi.a na kazi nzuri anayoifanya katika kuiongoza nchi. 

Alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka, kulinda mali za umma na kuhakikisha tofauti za maoni zinatatuliwa kwa njia za amani na kisheria.


No comments