Samia aipongeza Tanzanite Queens kwa kuingia fainali Kombe la Dunia




 RAIS Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Taifa ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ kwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Poland baadaye mwaka huu

Tanzanite Queens iliifunga Cameroon mabao 2-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja jana na kufuzu kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo kuwa 3-3 kwani katika mechi ya awali iliyochezwa jijini Yaoundé, Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Rais Samia aliandika; “Ninaipongeza timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens), kwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2026. Ushindi wenu ni historia na heshima kubwa kwa nchi yetu, ikiwa ni mara ya kwanza Tanzania kufuzu kushiriki mashindano hayo.

“Ninaielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na mamlaka zote zinazohusika kufanya maandalizi bora yatakayoiwezesha timu yetu kuiwakilisha vyema Tanzania na Afrika Mashariki katika mashindano hayo” alimaliza Rais Samia.

Tanzanite Queens imefikia rekodi iliyowahi kuwekwa na timu ya Taifa ya wanawake ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Girls' na ile ya timu ya taifa ya Wanawake ya Futsal ya kuwa timu pekee za taifa za Tanzania zilizowahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Serengeti Girls ilishiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 na kuishia katika hatua ya robo fainali wakati katika Futsal, Tanzania iliishia katika hatua ya makundi.

Kocha Mkuu wa Tanzanite Queens, Bakari Shime anaandika rekodi ya kuwa kocha pekee wa soka Tanzania kuwahi kuzipeleka timu mbili za taifa katika fainali za Kombe la Dunia mara ya kwanza aliiongoza Serengeti Girls kufuzu fainali zilizofanyika India.

Shime alisema haikuwa kazi rahisi bali akawapongeza wachezaji kwa kuichukua mechi kutoka Cameroon na kuja kuimaliza hapa nchini.

“Wachezaji wamejitolea, wameshindana kitu ambacho ilikuwa shida yetu kubwa kwenye mpira wa miguu wa wanawake kwa hiyo kiwango cha ushindani kilikuwa kidogo lakini kwenye mechi hii umeona tumeweza kuvumilia nguvu za wapinzani wetu na mwisho tukapata matokeo mazuri” alisema Shime.





No comments