RIO FERDINAND KUFUNGUA MILANGO YA ULAYA KWA VIJANA




Nahodha wa zamani wa England na klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand, amesema kuwa yeye si mwanasiasa na hajaja nchini kuzungumzia siasa, bali amekuja kuhamasisha vijana kupitia soka na hawezi kuzuiwa kuitembelea Afrika wala kuambiwa nini cha fanya. 

Katika ziara yake, Ferdinand ameahidi kushirikiana na kusaidia vijana wa Tanzania kupitia miradi ya maendeleo ya michezo na elimu, ambapo taasisi yake pamoja na wakala wake wa soka watafuatilia kwa karibu vipaji vya timu ya Tanzania ya umri wa chini ya miaka 17 wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Qatar.

Ujio huu unatajwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuwa utafungua fursa nyingi kwa vijana wenye vipaji nchini kwenda kucheza soka la kulipwa kwenye ligi kubwa za Ulaya kama vile Hispania, Ujerumani na England. Makonda alieleza kuwa ndoto yake haikuwa tu kuona Ferdinand anaposti kuhusu Tanzania kwenye mitandao ya kijamii, bali ilikuwa ni kumwona anafika nchini na kupitia kampuni yake, asaidie kuskauti vijana wazuri wa Kitanzania wenye vipaji ili waende kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Ferdinand alihitimisha ziara yake ya siku tatu jana baada ya kuwasili nchini Mei 19, ambapo alipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Uwanja wa Arusha, kukutana na viongozi mbalimbali, pamoja na kufanya mazoezi ya vitendo na vijana katika Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea nchini England.


No comments