Ushindani na Filamu za Kimataifa: ZIFF 2026 Kuleta Mapinduzi ya AI na Burudani Visiwani Zanzibar



JUMLA ya filamu 65 zimefanikiwa kuingia kwenye hatua ya ushindani katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) la msimu wa 29 kati ya kazi zaidi ya 400 zilizowasilishwa kutoka kote duniani. 

Katika mchanganuo huo wa filamu zilizochaguliwa, kundi la ushindani linajumuisha filamu fupi 22 zikiwemo kazi kutoka Tanzania kama vile Kilwa Kisiwani na Embe Dodo, filamu ndefu 14, filamu za makala 13, tamthilia za televisheni 10, pamoja na filamu 6 za vikaragosi.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa  tamasha, Khatibu Madudu,wakati akitangaza rasmi orodha ya filamu zitakazochuana vikali katika tamasha la mwaka huu jijini Dar es salaam  Mei 20 kwa waandishi wa habari.

Madudu alisema mnyukano huo mkali utakahusisha mataifa zaidi ya 100 yaliyotuma kazi zao, huku ukanda wa Afrika Mashariki pekee ukiingiza filamu 129 zilizochambuliwa kwa umakini mkubwa na jopo la majaji kabla ya kufikia hatua hii ya fainali, una hadhi ya kimataifa kutokana na ushiriki wake.  

Madudu alitaja uwapo wa filamu kadhaa za kipekee zitakazofanya onyesho lake la kwanza barani Afrika almaarufu kama 'African Premiere'ikiwamo About My Mom kutoka Uturuki, Prank (Jokes on You) kutoka Zambia, Nisamehe Baba kutoka Zanzibar, pamoja na filamu ya kikaragosi ya Princess Mkatu kutoka Uganda. 



Alisema uwepo wa filamu hizi za primia una maana kubwa sana kwa tamasha la ZIFF, kwani unalipandisha hadhi kimataifa na kulifanya kuwa soko kuu na kitovu cha kwanza cha ugunduzi wa kazi mpya za sanaa barani Afrika, jambo linalovutia wawekezaji, wasambazaji wa filamu, na wapenzi wa sinema kutoka pembe zote za dunia kuja Zanzibar kushuhudia ubunifu huo kabla haujafika kwingineko. 

Tamasha la mwaka huu litakalofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Juni 2026 visiwa vya Zanzibar, limebeba kaulimbiu isemayo “Akili Unde (AI) na Sanaa ya Usimuliaji wa Hadithi,” ambayo inalenga kuangazia mustakabali wa teknolojia katika tasnia ya filamu ya Kiafrika. 

Licha ya changamoto za miundombinu na rasilimaliwatu nchini, tamasha linatumika kama daraja la kujadili matumizi sahihi ya AI kupitia warsha mbalimbali zitakazoongozwa na wataalamu mahiri kama Lisa Russell na Robert Mwampembwa.

Kupunguzwa kwa siku za tamasha kutoka siku tisa hadi tano kutasaidia kuonyesha kazi zenye ubora wa hali ya juu pekee, huku kukiwa na matukio maalum ya kijamii kama vile ujio wa wanajamii 20 wa kabila la Wahadza watakaoshiriki kujadili filamu yao ya makala iitwayo “We Are Hadza” iliyoongozwa na Hannah Sparkman.

No comments