ARSENAL BINGWA! Angalia safari ya miaka 6 ya Arteta
Shangwe, vigelegele na nderemo za furaha zimerindima England na kote duniani baada ya Arsenal kutunukiwa rasmi ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2025/26 kufuatia kukwama kwa Man City kwa Bournemouth kwenye dimba la Vitality Stadium.
Kama wewe mpenzi wa washika bunduki hao unaweza kusema kwamba baada ya kusubiri kwa miaka 22 ukiwa na maumivu, ukidhihakiwa ubingwa huu umekuja kwa namna ya kusisimua mno baada ya wapinzani wako wakubwa, Manchester City, kulazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Bournemouth.
Katika mchezo huo Manchester City walihitaji kupata ushindi kwa udi na uvumba lakini Bournemouth walicheza mpira wa kiwango cha juu na kupata bao la kuongoza mnamo dakika ya 39 kupitia kwa kinda Eli Junior Kroupi aliyepiga shuti kali la upinde lililomwacha kipa Gianluigi Donnarumma hana la kufanya.
Ingawa Erling Haaland alifunga bao la kusawazisha dakika za lala salama baada ya mpira kugonga mwamba, muda ulikuwa umeshawatupa mkono mabingwa hao watetezi, huku mashabiki wao wakibaki wakiimba kumlilia kocha Pep Guardiola asiondoke mwishoni mwa msimu.
Safari ya Arsenal kuelekea kileleni haikuwa rahisi hata kidogo bali ilikuwa ya kupanda na kushuka, iliyojaa mawimbi mazito na majaribio ya kila namna.
Chini ya mradi wa miaka sita wa Mikel Arteta, timu hii ilipitia vipindi vigumu vya kukosa ubingwa katika hatua za mwisho kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, jambo lililowafanya wengi kuwabeza kama timu isiyoweza kumaliza kazi.
Hata katika msimu huu, Arsenal walikumbana na dhoruba ya kupoteza morali mwezi uliopita, wakapoteza fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Man City, na hata kufungwa tena kwenye ligi, hali iliyozua hofu kubwa ya mambo kuharibika tena dakika za mwisho.
Katikati ya dhoruba hizo, kocha Mikel Arteta alionyesha ufundi wa kipekee na mbinu za kisaikolojia zilizowaacha wengi midomo wazi ili kurudisha morali ya timu.
Katika kipindi kile cha kupoteza mwelekeo, Arteta aliwasha moto halisi kwenye uwanja wa mazoezi wa London Colney na kuwaomba wachezaji wake watupe mawazo yote hasi kwenye moto huo kwa njia ya mfano, huku akisisitiza kauli mbiu yake ya "make it happen" kupitia wimbo maalum wa AI uliopendwa sana na kikosi hicho.
Kutokana na mbinu hizo za kiubunifu, usajili wa nguvu wa pauni milioni 250 chini ya Mkurugenzi mpya wa Michezo Andrea Berta, na ujio wa mshambuliaji hatari Viktor Gyokeres aliyefunga mabao 14 ya ligi, Arsenal ilizinduka na kuwa mashine isiyozuilika.
Uimara wa mabeki kisiki William Saliba na Gabriel Magalhaes, pamoja na chuma cha katikati Declan Rice aliyepiga dakika nyingi zaidi uwanjani, uliipa Arsenal nguvu ya kupambana hadi sekunde ya mwisho.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto za majeraha, Arteta alijua jinsi ya kutumia vipaji vichanga kama vile chipukizi wa miaka 16 Max Dowman, ambaye amevunja rekodi zote msimu huu na kufananishwa na Lionel Messi kwa uwezo wake mkubwa. Kiukweli
mchanganyiko wa miamba ya kazi na damu changa ulitengeneza kikosi imara kilichoweza kuhimili shinikizo zote za Ligi Kuu ya England.
Mashabiki wa Arsenal wameeleza kuwa ubingwa huu ni ukombozi mkubwa baada ya miaka mingi ya maumivu na dhihaka za kukosa taji. Huku mkataba mpya wa Arteta ukiwa njiani na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League) dhidi ya PSG ikisubiriwa Mei 30 kule Budapest, Arsenal sasa wana fursa ya kujitangaza kama kikosi bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo.



Post a Comment