Kampeni ya ‘Never Again’ Kusambazwa Nchi Nzima: TAHLISO Kujenga Jeshi la Kulinda Amani na Utaifa
Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) imetangaza mkakati mzito wa kusambaza nchi nzima kampeni ya kizalendo ya ‘Never Again’ (Kamwe Haitatokea Tena). Hatua hiyo inalenga kuhamasisha amani, umoja, na mshikamano, huku ikipiga marufuku vitendo vyote vya vurugu na uvunjifu wa amani ambavyo vimekuwa vikitishia mustakabali wa Taifa.
Akizungumza kwa ari kubwa katika Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu jijini Dar es Salaam, Rais wa TAHLISO, Geofrey Kiliba, alibainisha kuwa kaulimbiu hiyo imekuja wakati muafaka ili kuwajenga vijana kisaikolojia kuwa walinzi wa kwanza wa maslahi ya nchi.
Kiliba alifafanua kuwa harakati hizo zilizaliwa mkoani Dodoma, zikiwa na ujumbe mzito wa kutoruhusu mtu yeyote—bila kujali nguvu au ushawishi wake—kuchezea misingi ya amani ya Tanzania.
"Wenzetu wa Dodoma walimaanisha hawako tayari kushuhudia mtu yeyote mwenye nguvu au akili timamu anayekusudia kuvunja msingi wa amani ya taifa letu. Wao walibeba dhamana ya kuwa mabalozi wa amani, umoja na mshikamano," alisema Kiliba.
Baada ya kuona ujumbe huo unaungwa mkono kwa dhati, viongozi wa TAHLISO walipanua wigo kwa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo ya waendesha bodaboda na vikundi vya mchakamchaka (jogging). Katika kuongeza nguvu, waliamua kuusambaza mkakati huo nchi nzima kwa kuongeza kauli mbiu mama ya: ‘Tuipende, Tuitunze na Tuilinde Tanzania.’
Katika kuunga mkono harakati hizo za vijana kivitendo, Serikali imekuja na mipango madhubuti ya kuwawezesha kiuchumi ili kuwepusha na vishawishi vya kisiasa.
Urasimishaji wa Fursa (Ubungo):
Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, alitangaza kuanza kwa mpango wa kurasimisha shughuli za vijana kuanzia Wilaya ya Ubungo, ambapo vijana 9,000 kutoka mitaa 90 watanufaika, huku wanafunzi 180 wa TAHLISO wakishirikishwa kusimamia utekelezaji wake.
Mtaji wa Shilingi Bilioni 1:
Serikali tayari imetoa kiasi cha Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufanikisha mpango huo kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mabadiliko ya Mfumo wa Elimu (K ya Nne):
Waziri Nanauka alieleza kuwa serikali imeongeza ‘K’ ya nne kwenye mfumo wa msingi wa elimu (Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu) ambayo sasa itakuwa ni ‘Kufanya Kazi’, ili kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Kauli za Viongozi: "Chungeni Amani, Wekeni Siasa Kando"
Viongozi waandamizi wa serikali waliohudhuria kongamano hilo walitoa nasaha zao nzito kwa wasomi hao.Profesa Paramagamba Kabudi (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu),alisisitiza kuwa amani ndiyo rasilimali kuu ya nchi na kuwataka vijana kuwa macho dhidi ya mbinu zozote zinazolenga kuchafua utulivu uliopo.
Aidha Albert Chalamila (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), aliwasihi wanafunzi wa vyuo vikuu kuachana na siasa zisizo na tija ambazo mara nyingi hutumiwa na wanasiasa kama ngazi ya maslahi binafsi. Badala yake, aliwataka kuweka nguvu zao zote kwenye masomo, nidhamu, na kujenga maisha yao kupitia kazi halali.
Post a Comment