SERENGETI BOYS YAINYUKA ANGOLA 3-0 NA KUKATA TIKETI YA KOMBE LA DUNIA




TIMU ya soka ya Taifa ya wavulana chini ya umri wa miaka 17, ‘Serengeti Boys’, imeandika ukurasa mpya wa kihistoria katika soka la Tanzania baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON-U17) na kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Angola, katika mchezo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Mohammed VI nchini Morocco.

Ushindi huo unaifanya Serengeti Boys kufikisha jumla ya pointi sita baada ya kushinda michezo miwili mfululizo, hatua inayoweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya wanaume nchini kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026. Hata hivyo, kihistoria hii inakuwa timu ya tatu ya taifa kufikia mafanikio hayo makubwa baada ya dada zao wa Serengeti Girls kufanya hivyo mwaka 2022, wakifuatiwa na Tanzanite Queens waliokata tiketi hiyo mapema mwaka huu.

Mabao yaliyowabeba vijana hao wa Kitanzania na kuwapeleka Qatar yalipatikana kupitia mashambulizi makali yaliyofungwa kwa umakini mkubwa na wachezaji Razaki Juma, Hassani Kizinga pamoja na Sadam Hussein, ambao walionyesha kiwango cha juu na nidhamu ya mchezo tangu dakika ya kwanza hadi ukamilisho wa mchezo huo dhidi ya Angola.



Baada ya kuwatoa nishai Angola, miamba hiyo ya Tanzania sasa imebakiza mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba ya makundi dhidi ya timu ya Taifa ya Mali, mchezo utakaopigwa Mei 20 mwaka huu. Mali ambayo kwa sasa ina pointi moja ilitarajiwa kucheza jana dhidi ya Msumbiji ambao hawana pointi yoyote katika kundi hilo, jambo linalofanya mchezo ujao kuwa wa vuta ni kuvute ya kukata na shoka.

Mtanange huo dhidi ya Mali, ambao walikuwa washindi wa pili katika mashindano yaliyopita, unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa wa aina yake kwani wapinzani hao watakuwa wanapambana kufa na kupona kusaka ushindi utakaowavusha, wakati Serengeti Boys nao wakiingia uwanjani kulinda heshima yao ya kutosalimisha pointi na kutoruhusu wavu wao kutikiswa katika hatua hii.

Mafanikio haya ya sasa yanakuja kama fidia na faraja kubwa kwa mashabiki wa soka nchini ikizingatiwa kuwa Serengeti Boys ilishiriki fainali hizo za Afrika katika miaka ya 2017, 2019 na 2025 lakini katika vipindi vyote hivyo iliishia kuondolewa mapema kwenye hatua ya makundi bila kuvuka mbele.



Katika mfumo wa mashindano ya mwaka huu, jumla ya timu 10 kutoka Afrika zitafuzu kucheza Kombe la Dunia, ambapo nafasi hizo zitatolewa kwa timu zitakazoshika nafasi za juu katika makundi manne ya michuano hiyo huku washindi watatu wa nafasi zinazofuata wakilazimika kucheza hatua ya mtoano ili kupata timu nyingine mbili zitakazokamilisha idadi hiyo ya timu kumi zinazokwenda Qatar

No comments