Kati ya 594 ni 18 tu wapenya Tuzo za EJAT
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetangaza orodha ya wateule 18 watakaowania Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa msimu wa 16, ambao ulihusisha uchujaji wa kazi za mwaka 2024 na 2025 kupitia mfumo mpya wa kidigitali.
Hatua hii kubwa na ya kihistoria imeshuhudia jopo la majaji 12 likitumia mfumo huo wa kisasa kufanyia tathmini jumla ya kazi 594 zilizowasilishwa katika makundi 11 tofauti.
Mfumo huu mpya wa kiteknolojia umeleta mapinduzi makubwa kwa kuanzisha hatua tatu kuu ambazo zimeongeza kiwango cha juu cha ubora na athari za kazi za kiandishi.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT , Ernest S. Sungura.
Katika mabadiliko hayo kwenye mchujo, hatua ya kwanza ilihusisha uchujaji wa kidigitali kabla ya kuwafikia majaji, ambapo kazi 60 ziliondolewa kiotomatiki kwa kukosa vigezo vya msingi. Hatua ya pili ilikuwa ni tathmini bila upendeleo ambapo alama pekee ndizo zilizoamua washindi pasipo kuwepo kwa majadiliano yoyote, huku hatua ya tatu ikitoa kipaumbele kwa kigezo cha ushahidi wa athari, ikilenga waandishi waliothibitisha kuwa habari zao zilileta mabadiliko halisi katika jamii.
"Kutokana na uchujaji huo mkali, idadi ya wateule msimu huu imeshuka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia 18 tu, tofauti na wastani wa wateule 30 hadi 35 wa miaka ya nyuma," alisema Sungura.
Kamati ya maandalizi imebainisha kuwa mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari pia yamechangia katika idadi na aina ya kazi zilizowasilishwa mwaka huu.
Kazi ya kuchakata mawasilisho hayo ilifanywa na jopo la majaji lililoongozwa na Mwenyekiti Jesse Kwayu na Katibu Mwanzo Millinga, wakisaidiana na wajumbe Absalom Kibanda, Neville Meena, Asha Dachi, Beatrice Bandawe, Hassan Mhelela, Joyce Shebe, Shifaa Said Hassan, Sauli Gilliard, Rashid Kejo, na Dkt. Egbert Mkoko.
Kwa Mujibu wa Sungura waandishi waliofanikiwa kuingia katika hatua hii ya fainali na vyombo vyao vya habari kwenye mabano ni Shaban Hamisi na Sanula Athanas (Nipashe), Simon Mkina (Pambazuko Online), Daniel Samson, Esau Ng'umbi na Kelvin Makwinya (Nukta Africa), Diki Kanyika (Sahara Media), Mackriner Siyovelwa (Crown Digital), Abel Kilumbu (EATV) na Francis Kajubi, Vitus Medard na Neema Abel (The Guardian).
Wengine ni Devotha Kihwelo (Mwananchi), Anthony Rwekaza (Watetezi Online TV), Isack Lukumay (Orkonerei FM), Joseph Kirati (The Chanzo), Abdallah Kurwa (ITV), pamoja na Huwaida Moh'd (Assalaam FM).
Kilele cha kinyang'anyiro hiki kikubwa kinatarajiwa kuwa Ijumaa, tarehe 29 Mei, 2026 kuanzia saa 10 jioni katika Ukumbi wa Four Points By Sheraton (New Africa) jijini Dar es Salaam ambapo matokeo rasmi yatatandazwa.
Sherehe hizo zitapambwa na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji Nestor Kayobera, ambaye atakuwa Mgeni Rasmi na atakayekuwa na heshima ya kumkabidhi tuzo Mshindi wa Jumla pamoja na Mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari (LAJA 2026).

Post a Comment