SAMIA AFUNGUKA NISHATI YA NYUKLIA BARANI AFRIKA




Na Mwandishi Maalum


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mwito kwa viongozi na wadau wa nishati barani Afrika kuhama kutoka kwenye nia na mikakati tu ya kupata nishati ya kutosha na kuingia katika hatua halisi ya utekelezaji wa miradi. 

Akizungumza wakati wa Mkutano wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA) uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, Rais Samia alieleza kuwa nishati ya nyuklia ni nguzo muhimu itakayosaidia bara la Afrika kupiga hatua kubwa kiuchumi na kiviwanda.

Alisisitiza kuwa mahitaji ya umeme nchini Tanzania yanaendelea kukua kwa kasi kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, na kwamba nchi hiyo inatazama teknolojia ibuka za nyuklia, kama vile vinu vidogo vya kisasa vya kuzalisha nishati, kama suluhisho thabiti la muda mrefu la kukabiliana na changamoto za nishati bila kuathiri juhudi za utunzaji wa mazingira.

Katika mkutano huo uliobeba kaulimbiu ya kuweka nia ya nishati ya nyuklia katika uwekezaji halisi, Rais Samia alibainisha kuwa matumizi salama na ya amani ya nishati hiyo yanahitaji mifumo thabiti ya kisheria, wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, pamoja na usimamizi madhubuti unaozingatia viwango vya kimataifa. 

Kufuatia misingi hiyo, Tanzania imekuwa ikifanya mazungumzo ya kimkakati na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rafael Mariano Grossi, ili kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya nishati hiyo, matibabu ya ugonjwa wa saratani, kilimo, na mifumo ya udhibiti kisheria. 

Serikali ya Tanzania imethibitisha utayari wake wa kuanzisha Taasisi ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Programu ya Nishati ya Nyuklia ili kusimamia azma hiyo kwa usalama na ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema mafanikio ya uchumi wa Afrika yanategemea uwezo wa bara hilo kujitosheleza kwa nishati, na kwamba nishati safi ya nyuklia si chaguo la maendeleo pekee, bali ni msingi mkuu wa ukuaji wa kisasa wa viwanda na ushindani wa kimataifa. 

Alisema Rwanda inaendelea na mipango yake ya kimkakati ya kuhakikisha nishati ya nyuklia inaanza kutumika ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2030, na kusisitiza kuwa Afrika haiwezi tena kutegemea vyanzo vya nishati visivyo na uhakika ikiwa inataka kushindana katika soko la dunia. 

“Kwa Afrika, nishati si suala la maendeleo pekee, ni msingi wa maendeleo ya viwanda na ushindani… ujenzi wa kisasa, uchakataji 

wa madini, miundombinu ya kidigitali na huduma za afya vyote vinategemea upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alieleza Rais Kagame. 

Alisema teknolojia mpya zitaongeza mahitaji ya umeme Afrika, akibainisha kuwa ukuaji wa haraka wa Akili Unde (AI) pamoja na mapinduzi ya kidijiti yataongeza matumizi ya nishati. 

“Nchi ambazo haziwezi kukidhi mahitaji hayo hazitaweza kushindana,” alionya.

 “Ndiyo maana nishati ya nyuklia ni sehemu muhimu ya mustakabali wa Afrika,” alisema Rais Kagame. Licha ya kukiri kuwa vyanzo vya nishati jadidifu kama jua na umeme wa maji vinaendelea kuwa muhimu kutokana na rasilimali.

 “Uchumi wetu hauwezi kuendeshwa kwa ufanisi kwa kutegemea nishati pekee inayokatika mara kwa mara,” alisema, na kusisitiza umuhimu wa kuwa na umeme wa uhakika wa msingi unaoweza kupatikana kupitia nishati ya nyuklia. 

Alisema watapeleka mjadala huo mpaka ufanikiwe na kuingia kwenye vitendo pamoja na mifumo ya kifedha inayoweza kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa. Mkutano huo unakutanisha viongozi wa Afrika, wataalamu wa nishati, wawekezaji na mashirika ya kimataifa kujadili nafasi ya nishati ya nyuklia katika kuleta maendeleo ya Bara la Afrika.

Mbali na masuala ya nyuklia, ziara hiyo ya kikazi nchini Rwanda imeshuhudia kuimarika kwa diplomasia ya kiuchumi kati ya nchi hizo mbili jirani baada ya kushuhudiwa kwa utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Nishati. 

Makubaliano hayo yaliyosainiwa na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Dkt. Jimmy Gasore, mbele ya Rais Samia na mwenyeji wake Rais Paul Kagame, yanaweka msingi imara wa ushirikiano katika usafirishaji wa umeme, mafuta, maendeleo ya gesi asilia, ulinzi wa mifumo ya kidigitali, na matumizi ya akili mnemba katika mifumo ya nishati. 


No comments