Nsanganzelu ataja 25 kuunda Kikosi Serengeti Boys Afcon




KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya wavulana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu ametaja kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U17) inayotarajiwa kuchezwa Morocco kuanzia Mei 13 hadi Juni 2, mwaka huu. 

Serengeti Boys iko Kundi C lenye timu za Angola, Msumbiji na Mali ambao ni washindi wa pili katika mashindano yaliyopita. 

Nsanganzelu aliwaita wachezaji wengi kutoka katika Programu ya Kuendeleza Vipaji (TDS) wakati klabu za Azam, Yanga na Simba zikitoa wachezaji wachache. 

Kikosi hicho kinawajumuisha Abrahman Nassoro, Ismail Likungilo na Rajabu Manyelezi (Azam), Omary Yahaya na George Mzungu (Yanga), Haji Abdalah, Dismas Athanasi, Kassim Juma, Abdul Issa, Hassan Mkindai, Erick Yusuph, Idrisa Kilendem na Razaki Mbegelendi. 

Wengine ni Hassan Kizinga, Hamis Mihambo, Hamisi Barua, Abbas Nasser, Issa Chole, Sadam Hamis, Sultan Silver na Nhingo Luzengela (wote TDS). Pia, Luqman Mbalasalu (Kagera Sugar) Abbas Nasser (African Sports), Issa Chole (Fountain Gate), Hussein Mbegu (Simba) na Soann Shabani (Grenoble Foot 38 ya Ufaransa). 

Timu hiyo iliyokuwa kambini Arusha, juzi ilicheza mchezo wa kirafiki na Cameroon na kushinda kwa mabao 3-1. 

Mashindano ya mwaka huu yatachezwa chini ya muundo mpya ulioanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), huku mechi nyingi na shughuli za timu zikiwekwa katika Uwanja wa Mohammed VI nchini Morocco. 

Ratiba muhimu pekee kama vile mechi ya ufunguzi, nusu fainali na fainali ndiyo itakayopangwa katika viwanja vingine. 

Muundo huo umeundwa ili kuboresha ukuzaji wa wachezaji, kurahisisha uratibu na kuhakikisha hali za kucheza zisizobadilika katika kipindi chote cha shindano. 

Timu nane bora zitafuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia la FIFA U-17 nchini Qatar, wakati timu zilizoshika nafasi ya tatu zitapata nafasi nyingine ya mchujo. Kundi la Serengeti Boys (Kundi C) ni Mali, Angola na Msumbiji na Kundi A ni Morocco (wenyeji), Tunisia, Misri na Ethiopia. Kundi B ni Ivory Coast, Cameroon, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Kundi D ni Senegal, Afrika Kusini, Algeria na Ghana.


No comments