Bilionea wa Utalii Manfred Lefebvre Aahidi Kuongeza Uwekezaji Tanzania



Bilionea na mmiliki wa kampuni maarufu ya utalii duniani ya Abercrombie and Kent, Bw Manfred Lefebvre amemwagia sifa utendaji wa sekta ya utalii nchini Tanzania na kuahidi kupanua wigo wa uwekezaji wake nchini humu. 

Bw Manfred ametoa kauli hiyo  Ijumaa Mei 8 mwaka 2026 wakati wa mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbasi yaliyofanyika pembeni mwa Mkutano wa Viongozi wa Sekta ndani ya meli yake ya kitalii inayotoka Port Said kwenda Alexandria nchini Misri. 

Mfanyabiashara huyo mkubwa amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri zaidi barani Afrika huku akipongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika kukuza utalii tangu kipindi cha uzinduzi wa filamu ya Royal Tour jijini New York.

Kampuni ya Abercrombie and Kent kupitia kampuni yake tanzu ya Crystal Cruises tayari imekuwa mdau mkubwa nchini Tanzania kwa kuleta maelfu ya watalii wanaotembelea maeneo ya Zanzibar, Kilwa na Dar es Salaam kwa kutumia meli za kifahari. 

Katika mazungumzo hayo Dkt Hassan Abbasi amemhakikishia bilionea huyo kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika mipango yake yote ya kuongeza uwekezaji ili kukuza zaidi sekta hiyo. 

Hatua hii inaashiria kuimarika kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa kwa Tanzania kama kitovu kikuu cha utalii barani Afrika kutokana na jitihada za makusudi za kuitangaza nchi na kuboresha mazingira ya biashara.

No comments