Hayati Mkapa na Ujumbe Wake wa Amani: Msingi wa Maendeleo ya Taifa




Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, aliongoza nchi kuanzia mwaka 1995 hadi 2005. Kipindi chake kiliambatana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa. Amani ilikuwa moja ya kipaumbele chake katika kipindi chote na hali hiyo imeendelea hata sasa Awamu Sita chini ya Uongozi mahiri wa Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mkapa alisisitiza mara kwa mara kwamba bila amani, hakuna uwekezaji, hakuna elimu, hakuna afya. Kwa maneno yake:  “Nchi isiyo na amani ni nchi inayojenga juu ya mchanga.”  Aliona amani sio jambo la kusubiri litokee, bali ni kitu kinachopaswa kulindwa kila siku.

Katika kipindi chake, Tanzania iliendelea hata sasa bado imebaki kuwa kitovu cha amani kwa nchi jirani. Mkapa alihusika moja kwa moja katika mazungumzo ya Burundi na Sudan Kusini. Aliamini kwamba bunduki haisuluhishi migogoro – mazungumzo ndiyo suluhu.

Ndani ya nchi pia, aliwataka Watanzania wajifunze kutofautiana kwa heshima. Alisema siasa ya matusi na chuki inaharibu zaidi kuliko inavyojenga.

Urithi mkubwa alioacha Mkapa ni imani kwamba Tanzania ni “kisiwa cha amani”. Alikazia kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na tofauti zetu za lugha, dini, na kabila si sababu ya kutugawa.

Kwa Mkapa, amani haikuwa kauli tu. Ilikuwa sera, ilikuwa utamaduni, na ilikuwa njia ya kufungua milango ya maendeleo. Ujumbe wake unabaki kuwa muhimu leo: tukilinda amani, tunaweka msingi imara wa mustakabali wetu.

No comments