Makumbusho ya Kwanza ya Muziki na Nyaraka Kufunguliwa Rasmi Kulinda Urithi wa Kizazi Kipya



Makumbusho ya Elimu ya Muziki na Uhifadhi wa Nyaraka za Utamaduni wa Zanzibar, hatua inayolenga kutengeneza makazi salama ya nyimbo, vyombo vya muziki, picha na historia za magwiji wa sanaa ya asili yanafunguliwa Mei 19  mjini Zanzibar. 

Taarifa ya mkuu wa chuo Halda Alkanaan ilifafanua kuwa makumbusho hayo ni ya kwanza ya aina yake visiwani Zanzibar, ikiwa ni hatua nyingine kubwa katika kulinda urithi wa sanaa na kufungua milango ya elimu, utafiti, na ubunifu kwa dunia nzima.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Chuo cha Muziki cha Nchi za Jahazi (DCMA), eneo hili jipya litakuwa kitovu cha kuhifadhi taarab asilia, kidumbaki, ngoma, beni, vikundi vya muziki, na hadithi za urithi wa utamaduni ili kuhakikisha hazipotei bali zinasalia kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. 

Mkuu huyo alibainisha kuwa makumbusho haya si jengo tu la kuhifadhi vitu vya kale, bali ni nyumba hai ya kumbukumbu, elimu, na utambulisho wa Wazanzibari ambapo ndani yake zitasikika sauti za kihistoria na kuhifadhiwa vyombo vilivyobeba ujumbe wa jamii kwa miaka mingi.

Uongozi wa chuo hicho umeeleza kuwa kwa muda mrefu mradi huo ulikuwa ndoto ya dhati ya taasisi hiyo katika kuona uwepo wa sehemu maalum ya kuenzi utamaduni, na sasa maono hayo yametimia kwa kishindo. 

Mkuu wa chuo alitoa shukurani za kipekee kwa taasisi ya Creation Africa kupitia Ubalozi wa Ufaransa na Alliance Française kwa msaada mkubwa wa kuboresha makumbusho hayo, pamoja na Unesco Tanzania, Sanze, na Bodi ya Wadhamini ya DCMA chini ya Mwenyekiti wake, Bi Salma Adim. 

Aidha, chuo kilitambua mchango mkubwa wa wadau kama John Kagaruki, Mohamed Muombwa, na hasa Khamis Mohamed Kizoro aliyetumia muda mwingi kubuni na kupanga makumbusho hayo bila kukata tamaa licha ya changamoto za kupata jengo lenye nafasi, sambamba na mchango wa wafanyakazi, walimu, na wanafunzi waliofanikisha jambo hilo.

Chuo cha Muziki DCMA, kikiwa ni taasisi isiyo ya kiserikali na chuo cha aina yake cha kipekee nchini kinachotoa mafunzo ya muziki, kimeendelea kudhihirisha umuhimu wake katika kuhifadhi, kutangaza, na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar ikiwemo muziki wa taarab, kidumbaki, ngoma, na beni. 

No comments