Wino wamwagwa Miss World 2027 Kuwa Tanzania


Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shindano la Mrembo wa Dunia, Julia Morley wakionesha mkataba waliosaini wa kuandaa shindano hilo 2027 katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam jana. Anayeshuhudia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda.


Na Mwandishi Wetu BSKY Media

Historia imeandikwa rasmi baada ya Tanzania kupewa kiti cha kuwa mwenyeji wa shindano la 74 la Miss World 2027, hatua inayopiga muhuri wa dhahabu nafasi ya nchi kwenye ramani ya kimataifa ya utalii na burudani. 

Leo Aprili 20 nchi ilisimama kwa muda wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipoangusha wino kusaini mkataba huo wa kihistoria. Tukio hilo lilishuhudiwa na Waziri wa Habari, Paul Makonda, na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samweli Maneno, ni ushahidi tosha kuwa ulimwengu sasa unaiinamia Tanzania kwa heshima na weledi wake.

Waziri Paul Makonda amemwaga cheche akisema Tanzania imefanya mapinduzi makubwa kwa kuwa nchi ya tatu pekee barani Afrika kuwahi kuandaa shindano hili kubwa tangu lilipoanzishwa mwaka 1951, ikizifuata Afrika Kusini na Shelisheli. 

Shindano hilo ambalo litadumu kwa siku 28 za moto, litafanyika katikati ya mandhari ya kito na paradiso ya Kitanzania, likiifungua nchi kwenye fursa lukuki za kiuchumi na kijamii. Hii si tu habari ya urembo, bali ni mlango mkuu wa kuvutia wawekezaji na watalii ambao watamiminika kutoka mataifa zaidi ya 100 duniani kote.

Msisimko huo unatarajiwa kuamsha ari ya maandalizi ya kufa na kupona kuanzia sasa ili kuhakikisha kuwa ugeni huo mzito unashuhudia ubunifu na ukarimu wa kipekee wa Mtanzania. 

Hatua hii inatabiriwa kuchochea ukuaji wa ajira kwa vijana na kuitikisa sekta ya sanaa kwa namna ambayo haijawahi kutokea. Kuaminiwa kwa Tanzania kuandaa tamasha hili la mwezi mzima ni ishara kuwa dunia ina imani isiyotikisika na uwezo wa serikali yetu kuratibu matukio makubwa ya kimataifa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Hafla hiyo iliyosheheni nakshi za urembo ilishuhudiwa na warembo wenye majina makubwa duniani wakiwemo Miss World Tanzania Latricia Ian, Miss World Opal Suchata Chuangsri, na Miss World Afrika Hasset Dereje. 

Uwepo wa nyota hawa umeongeza hamasa ya kuwa Tanzania iko tayari kuonyesha dunia kile inachoweza kufanya. Ni mwanzo wa safari mpya ya kuitangaza nchi yetu kama kitovu cha urembo, utamaduni, na utulivu wa kudumu, huku kila mmoja akisubiri kwa hamu kishindo cha mwaka 2027.

No comments