Waziri Mkuu Dk. Mwigulu: Kataeni Wanaotaka Kuligawa Taifa kwa Siasa na Dini
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba ametoa mwito mzito kwa Watanzania kusimama imara na kukataa majaribio yoyote ya kuigawa nchi, akionya kuwa kuna watu wanatafuta mwanya kupitia siasa na dini ili kuvuruga umoja wa kitaifa.
Akizungumza na wananchi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Msanga wilayani Chamwino,Katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo, Dk. Mwigulu amebainisha kuwa baada ya mbinu za ukabila kushindwa, maadui wa maendeleo sasa wameelekeza nguvu zao kwenye maeneo hayo nyeti ili kuleta mifarakano itakayowawezesha kunufaika na utajiri wa rasilimali za nchi.
Dk. Mwigulu ameeleza kuwa kasi ya maendeleo ya Tanzania, ikijumuisha miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), imeyafanya baadhi ya mataifa kuingiwa na wivu na kutamani kuona nchi ikiyumba.
Amewakumbusha wananchi kuwa si kila mtu anafurahia hatua hizi za kishujaa ambazo serikali imezichukua, akisisitiza kuwa umoja na amani ndizo ngao pekee zitakazohakikisha miradi hiyo inaleta tija iliyokusudiwa kwa manufaa ya Watanzania wote.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu pia ametoa maelekezo ya kiutendaji akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino kuwasilisha bajeti ya kukamilisha majengo ya Hospitali ya Uhuru ili ianze kutoa huduma kama hospitali ya wilaya.
Post a Comment