CCM yampitisha Kaganda kugombea Ismani, Vunjabei, Kiswaga wapigwa chini
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Emmanuela Kaganda kuwa mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Ismani mkoani Iringa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Juni Mosi 2026.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.
Kabla ya uteuzi huo, Emmanuela alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, na aliwahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Awali katika kura za maoni Mfanyabiashara Fred Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei, aliongoza kwa kupata kura 2,703, lakini amewekwa kando katika uteuzi wa mwisho wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Emmanuela ambaye katika kura za maoni alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 621 amekuwa chaguo la CCM baada ya kupitishwa katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi wa mgombea wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Isimani, lililopo Wilaya ya Iringa Vijijini. Mgombea aliyeteuliwa ni Emmanuela Kaganda Mtatifikolo,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika matokeo ya kura za maoni yaliyoshirikisha wagombea 18, Vunjabei aliongoza akifuatiwa na Festo Kiswaga aliyepata kura 873, huku Mtatifikolo akishika nafasi ya tatu.

Post a Comment