WILLIAM LUKUVI: NI MWALIMU WA SIASA NA NGUZO MUHIMU YA UONGOZI





Viongozi mbalimbali nchini wameungana na Rais Samia Suluhu Hassan kumlilia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),William Vangimembe Lukuvi, wakimtaja kama nguzo muhimu ya uongozi na mwalimu wa siasa.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, na Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, wamemwelezea marehemu kama kiongozi mzoefu aliyetoa mchango mkubwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi. 

Hali kadhalika, mawaziri na wabunge wenzake wamemkumbuka kwa jinsi alivyokuwa akiwaunganisha viongozi wa Mkoa wa Iringa kupambania miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara za kuelekea mbuga ya wanyama ya Ruaha na miradi mikubwa ya umwagiliaji.

Taarifa ya kifo iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ilishtua wengi kuhusu kifo cha mmoja wa viongozi wakongwe aliyebeba historia ndefu ya utumishi wa umma, William Vangimembe Lukuvi. 

Alisema kwamba Saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, ndipo maisha ya mwanasiasa huyo mkongwe yalipofikia tamati akiwa na umri wa miaka 70, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Ndani ya muda mfupi, taarifa hiyo ilienea nchi nzima, ikiacha simanzi na kumbukumbu za mchango wake mkubwa kwa taifa akiwa ndiye mbunge pekee aliyekaa bungeni muda mrefu zaidi tangu mwaka 1995.

Hadi umauti unamfika, Lukuvi alikuwa ametumikia Jimbo la Uchaguzi la Isimani mkoani Iringa kwa miaka zaidi ya 30, akijipambanua kama kiongozi mchapakazi, mzalendo, na mshauri mahiri. 

Rais Samia Suluhu Hassan, katika salamu zake za rambirambi, amemwelezea Lukuvi kama kiongozi shupavu na mtumishi wa umma aliyelitumikia taifa kwa uadilifu na kujitolea. Rais alibainisha kuwa kifo hicho ni pigo kubwa kwa kuwa taifa limepoteza kiongozi mwenye uzoefu mkubwa ambaye mchango wake katika ujenzi wa maendeleo utaendelea kuenziwa na kukumbukwa na vizazi vingi vijavyo.

William Vangimembe Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955, katika Kijiji cha Mapogoro, Iringa, na alianza safari yake kama mwalimu kabla ya kujiunga na harakati za kisiasa. Alihudumu katika nafasi mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Dar es Salaam, na baadaye kushika nyadhifa za uwaziri. Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alijijengea heshima kubwa kwa ujasiri wake wa kutatua migogoro ya ardhi ana kwa ana na wananchi, akifuta hati za mashamba makubwa yasiyoendelezwa na kuyarudisha kwa wananchi wa kawaida.

Hadi dakika zake za mwisho, Lukuvi alikuwa bado ni mhimili wa shughuli za serikali bungeni akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). 

Juzi tu, kabla ya mauti kumfika, alikuwa akishirikiana na viongozi wenzake kuandaa vikao vya kitaifa, jambo linalothibitisha kuwa alitumikia taifa lake kwa nguvu zake zote hadi pumzi ya mwisho. 

Kutokana na msiba huu, Spika wa Bunge aliahirisha vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge ili kutoa nafasi kwa maombolezo, huku historia ikimwandika Lukuvi kama kiongozi aliyeacha alama zisizofutika katika mioyo ya Watanzania.

No comments