Wauguzi 300 Kupata Ajira Saudi Arabia Mwezi Aprili




Serikali imetangaza neema kwa wahitimu wa fani ya uuguzi nchini, baada ya kubainisha kuwa mapema mwezi Aprili 2026, itatangaza fursa za ajira 300 kwa ajili ya wauguzi wa Kitanzania kwenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia.

Tangazo hilo limetolewa jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, wakati wa hafla ya kuaga kundi la vijana 521 wanaokwenda kufanya kazi katika mataifa mbalimbali ughaibuni, 45 wakienda bara la Ulaya zikiwemo nchi za Denmark,Poland, Bosnia na Ujerumani.

Mhe. Sangu ameeleza kuwa fursa hizo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Tanzania na Wizara ya Afya ya nchi ya Saudi Arabia. Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za makusudi za Serikali ya awamu ya sita kupanua masoko ya ajira ya kimataifa kwa wataalamu wa Kitanzania, hususan katika sekta ya afya ambayo ina uhitaji mkubwa wa nguvu kazi yenye ujuzi na weledi duniani.

"Mapema mwezi Aprili, Serikali kwa kushirikiana na wakala husika inatarajia kutangaza kupitia vyombo vya habari fursa 300 za ajira kwa wauguzi wa Kitanzania watakaokwenda kufanya kazi katika Wizara ya Afya ya nchi ya Saudi Arabia," alisema Mhe. Sangu.

Waziri Sangu ametoa wito mahususi kwa wauguzi wote wenye sifa stahiki kuchamkia fursa hiyo pindi tangazo rasmi litakapotolewa. Alisisitiza kuwa wataalamu wa afya wa Tanzania wana uwezo mkubwa, nidhamu, na weledi unaotambulika kimataifa, hivyo nafasi hizo zitasaidia kuongeza uzoefu wao wa kitaaluma na kuboresha kipato chao.

Aliongeza kuwa mbali na kuongeza kipato, ujuzi watakaoupata huko ughaibuni utakuwa rasilimali muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya nchini Tanzania pindi wataporejea.

Aidha, Waziri amewatahadharisha vijana wanaotafuta fursa hizo kutumia njia rasmi zinazotambuliwa na Serikali na mawakala waliosajiliwa. 

Tangu Julai 2025 hadi Machi 2026, takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya Watanzania 6,246 wamefanikiwa kuunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi kupitia mawakala binafsi 18 na jitihada za Serikali, jambo linaloashiria kukua kwa diplomasia ya uchumi ya nchi inayosimamiwa na kutekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

No comments