Serikali Yaaga Vijana 521 Kwenda Kufanya Kazi Nje ya Nchi; 45 Waelekea Ulaya
SERIKALI ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imezidi kufungua milango ya ajira kimataifa baada ya kuwaaga jumla ya vijana 521 wanaokwenda kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani, zikiwemo nchi za bara la Ulaya.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kihistoria Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amewataka vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, na nidhamu ya hali ya juu.
Katika hotuba yake, Mhe. Sangu amebainisha kuwa tangu Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya Watanzania 6,246 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi kupitia mawakala binafsi na kwa juhudi za Serikali.
Kwa kundi hilo la sasa la vijana 521 wanakwenda Saudi Arabia, Qatar, Oman, UAE, Bahrain, na Kuwait. Wengine wanakwenda Denmark, Poland, Romania, Ujerumani, na Bosnia .
katika kundi hilo wapo vijana 45 wakiwemo wataalamu wa kilimo, mitambo na mafunzi wanakwenda katika nchi za bara la Ulaya. Aidha fursa zingine zimepatikana Guyana, Mauritius, na Canada.
Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Ajira , Jeni Sogoro, ameeleza kuwa mafanikio makubwa yanayopatrikana sasa katika fursa hizo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na mawakala binafsi 18 waliosajiliwa, ambao wamewezesha vijana kupata kazi katika kada mbalimbali kama vile afya, ujenzi, hoteli, udereva, na uhandisi.
Naye Meneja wa Hifadhi Scheme kutoka NSSF, Rehema Chuma (akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu), amesisitiza umuhimu wa vijana hao kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii.
Alibainisha kuwa NSSF imetoa elimu maalum ili vijana waweze kujidunduliza kwa ajili ya uzee, matibabu, uzazi, na kinga dhidi ya ulemavu. Hadi sasa, wanachama 290 wameshapata elimu hiyo, huku 45 wakijiunga rasmi siku ya Machi 27.
Kwa upande wa kifedha, mwakilishi wa Benki ya CRDB, Davinner Kweka, amewahimiza vijana hao kutumia "Diaspora Account" ambayo itawawezesha kuweka akiba, kupata mikopo, na kuwekeza nyumbani Tanzania wakiwa bado ughaibuni. Benki hiyo imeahidi kutoa huduma saa 24 kwa siku saba za wiki (24/7) ili kuwafikia popote walipo.
Aidha katika haflka hiyo Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala wa Ajira nchini, Abdallah Ahmed, ameishukuru serikali kwa diplomasia ya uchumi inayofungua fursa hizo.
Hata hivyo, mwakilishi wa mawakala, Patrick Kawogo, ametoa ombi kwa Serikali kufikiria kuanzisha Mfuko Maalum (Revolving Fund) utakaosaidia kugharamia vijana wenye sifa lakini wasio na uwezo wa kulipia gharama za awali za kusafiri (process costs), ambapo fedha hizo zitarejeshwa pindi wakianza kazi kutokana na vipato vizuri wanavyopata.
Mhe. Sangu ametoa onyo kali kwa mawakala wasio rasmi na kuwataka vijana kutumia njia halali ili kulinda usalama na haki zao. Pia, ametumia fursa hiyo kutangaza kuwa mapema mwezi Aprili 2026, Serikali itatangaza fursa nyingine 300 za wauguzi (nurses) wanaohitajika kwenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia.
"Ninyi ni mabalozi wa Tanzania; mnaibeba heshima ya Taifa letu. Mkifanya vyema, mnafungua milango kwa maelfu ya vijana wengine wa Kitanzania watakaokuja baada yenu," alihitimisha Mhe. Sangu.
Miongoni mwa vijana wanaoelekea ughaibuni ni wahitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Reila Shaban na Mussa Fanuel, ambao wameeleza kufurahishwa na fursa hizo wakiamini zitawapa nafasi kubwa ya kukua kiteknolojia kulingana na nchi wanazokwenda.
Reila Shaban, ambaye anaelekea nchini Denmark, amewataka mabinti wenzake nchini wasibweteke, bali wajibidii kutafuta fursa kwani zipo. Amesema ana matumaini makubwa ya kuongeza ujuzi na ufanisi katika elimu yake, akibainisha kuwa Denmark ni miongoni mwa mataifa yenye teknolojia ya juu duniani katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mussa Fanuel anayeelekea Ujerumani, amesema amefanikiwa kupata fursa hiyo kupitia wakala binafsi na ana matumaini ya kujipatia kipato cha kujiendeleza, huku akinoa zaidi utaalamu wake katika masuala ya Uchumi wa Kilimo (Agricultural Economics).
Naye kijana Mayunga Isaya, anayejiandaa kuelekea Denmark, amesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu halali za Serikali.
"Naondoka rasmi na wala sipitii njia za vichochoro. Nawataka vijana wenzangu Watanzania kutambua kuwa fursa zipo, kinachotakiwa ni kuzipambania kwa kufuata mifumo rasmi," alisema Mayunga.
mwisho
Post a Comment