UKOMAVU WA KISIASA: TANZANIA YAISHANGAZA DUNIA MAGEUZI YA KIDEMOKRASIA
TANZANIA imetoa tamko zito mbele ya Jumuiya ya Madola, ikithibitisha ukomavu wake wa kisiasa na dhamira ya dhati ya kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia yanayozingatia misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu.
Uthibitisho huo umetolewa katika Mkutano wa 72 wa Kikosikazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CMAG) uliofanyika jijini London, Uingereza, chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malta, Dk. Ian Borg.
Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Palamagamba Kabudi, uliwasilisha taswira ya nchi inayojitathmini na kuchukua hatua madhubuti za kurekebisha mifumo yake.
Profesa Kabudi alifafanua kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania inatekeleza mfumo wa kitaifa wa Kurekebisha, Kujenga Upya na Kurejesha (4R’s). Mfumo huu unalenga:
Kuimarisha taasisi za kidemokrasia.
Kukuza maridhiano ya kitaifa yasiyo na ubaguzi.
Kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao.
Tume ya Jaji Chande
Katika mkutano huo, Tanzania iliweka wazi uwazi wake (transparency) kwa kuelezea kazi inayofanywa na Tume Huru ya Uchunguzi chini ya Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman. Tume hiyo inachunguza matukio ya Oktoba 29, 2025, ikiwa ni sehemu ya kuwajibika na kutafuta ukweli.
Vilevile, Profesa Kabudi alitangaza maandalizi ya kuanzishwa kwa Tume ya Kitaifa ya Maridhiano, chombo kitakachokuwa injini ya mazungumzo ya kitaifa na mlinzi wa amani na mshikamano wa Watanzania.
“Mageuzi yanayoendelea nchini ni kielelezo cha utamaduni wetu wa muda mrefu wa amani. Hatufanyi haya kwa shinikizo, bali kwa imani kuwa demokrasia ndiyo msingi wa maendeleo yetu,” alisema Profesa Kabudi.
Jumuiya ya Madola Yaridhishwa
Kikosikazi cha CMAG kimepokea kwa kuridhika ripoti ya Tanzania, kikisifu hatua za ujasiri zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, Tanzania imeelezea utayari wake wa kumpokea Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola pindi taratibu za ndani, ikiwemo ripoti ya Jaji Chande, zitakapokamilika.
Post a Comment