ATCL YAFANIKISHA WATANZANIA 236 KUREJEA KUTOKA JEHENAMU YA VITA DUBAI
Hatimaye nyuso za tabasamu na machozi ya furaha zilitanda kwa abiria Watanzania 236 waliokuwa wamekwama jijini Dubai kutokana na mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati, kuwasili salama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Katika hali inayoonyesha kujali kwa Serikali, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilipeleka ndege maalum kubwa (Boeing) kuchukua raia hao, likiweka kando taratibu za kawaida za kibiashara ili kuokoa maisha ya Watanzania waliokuwa mashakani.
"Niliona Milipuko Kwa Macho Yangu"
Simulizi za abiria hao zimetawaliwa na hofu kubwa ya usalama. Mmoja wa abiria (jina limehifadhiwa) aliyekuwa ameenda Dubai kwa ajili ya sherehe ya kuzaliwa, alielezea namna safari ya siku tatu ilivyogeuka kuwa "ndoto ya kutisha" ya siku 13.
"Ukiwa kule huwezi kujua kama uko salama. Unatuma macho angani na kuona silaha zikitawala na milipuko ikitokea. Nimejifunza kwa mara ya kwanza madhara ya vita. Watanzania tulinde tunu yetu ya amani, si ya mchezo kabisa," alisema abiria mwingine kwa hisia kali.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ATCL, safari hiyo haikuwa ya kutafuta faida bali ilikuwa ni safari ya uokoaji. Shirika hilo liliamua kutumia ndege kubwa ambayo kwa kawaida haiendi ruti ya Dubai ili kuhakikisha idadi kubwa ya abiria waliokuwa na tiketi za safari zilizositishwa wanapata nafasi ya kurejea mara moja.
Ingawa abiria walitakiwa kulipia gharama, ATCL imebainisha kuwa gharama hizo zilikuwa nafuu na rafiki (affordable) ili kurahisisha urejeaji wa raia hao bila kuongeza mzigo wa kifedha wakati wa dharura.
Tukio hili linaonyesha uwezo wa nchi yetu kujibu mapigo wakati wa majanga ya kimataifa, huku likituachia funzo kuwa Amani ni Tunu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.

Post a Comment