TRILIONI MOJA KUIMARISHA UCHUKUZI MAZIWA MAKUU
Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuubadilisha
muonekano wa sekta ya uchukuzi nchini kwa kuwekeza kiasi kikubwa cha zaidi ya
shilingi trilioni moja katika miradi ya usafiri wa majini.
Msemaji Mkuu wa
Serikali, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Ndugu
Gerson Msigwa, amebainisha kuwa uwekezaji huo mkubwa unalenga kununua meli
mpya, kukarabati zilizopo, na kuboresha miundombinu ya bandari katika maziwa
makuu ya Victoria, Tanganyika, Nyasa, na ukanda wa Bahari ya Hindi.
Akizungumza na
waandishi wa habari machi 22,2026 alisema hatua hii ni sehemu ya mkakati wa
serikali wa kuunganisha huduma za usafirishaji na reli ya kisasa ya SGR ili
kujenga ushoroba wa kati wenye tija, ambao ni kiungo muhimu kwa nchi jirani
zisizo na bahari kama Uganda, DRC, na Burundi.
Kupitia uwekezaji
huu, Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha biashara kikanda, jambo litakalochochea
ukuaji wa pato la taifa na kuimarisha ushindani wa bidhaa za ndani katika
masoko ya kimataifa.
Akizungumza akiwa
mkoani Mwanza, Msigwa alisisitiza kuwa kukamilika kwa meli kubwa ya MV Mwanza
'Hapa Kazi Tu' kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 120 ni kielelezo cha
mafanikio hayo, ambapo meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400
za mizigo.
Aidha, serikali
inaendelea na ujenzi wa meli nyingine mpya ya mizigo katika Ziwa Victoria
itakayobeba tani 3,000 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 145.4.
Miradi hii inakwenda
sambamba na ukarabati wa meli za kimkakati kama MV Umoja uliogharimu dola za
Marekani 8,830,521.62 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 22.9 na MT Ukerewe
unaogharimu Shilingi bilioni 7.5.
Uwekezaji huu siyo tu
unaimarisha sekta ya uchukuzi, bali pia unashusha gharama za usafirishaji kwa
wafanyabiashara ikilinganishwa na usafiri wa barabara, hali inayopunguza bei za
bidhaa kwa mlaji wa mwisho na kukuza uchumi wa kaya.
Post a Comment