TUTUBA: TANZANIA IPO IMARA, VIJANA CHANGAMKIENI FURSA
Katika kipindi hiki ambacho mivutano ya kijiopolitika nchini Mashariki ya Kati (hususan kati ya Iran na Israel) inatikisa soko la dunia, ni rahisi kukumbwa na hofu. Hata hivyo, ujumbe wa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba, ni wa matumaini: Tanzania ipo salama.
Gavana anasema kwamba serikali imejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa hata kama mambo yataharibika huko nje, ndani ya nchi kuna "mto" wa kutokea (buffer). Hii inaashiria utulivu ambao ni muhimu kwa vijana wanaopanga kuwekeza au kuanza biashara.
Moja ya hofu kubwa ya vita ya Mashariki ya Kati ni kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, jambo ambalo limepandisha bei ya mafuta duniani.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, serikali haisubiri janga litokee; tayari mikakati ya kutumia Gesi Asilia (CNG) kwenye magari na mitambo imeanza kushika kasi. Ujenzi wa matangi makubwa ya kuhifadhia mafuta bandarini na vituo vya gesi ni hatua za makusudi kuhakikisha nishati haikosekani.
Wakati mataifa mengi yakihaha kudhibiti mdororo, uchumi wa Tanzania unaendelea kupaa. Takwimu za mwaka 2025 zinaonesha ukuaji wa 6% kwa Bara na 6.8% kwa Zanzibar, huku makadirio ya 2026 yakitabiri utulivu wa zaidi ya 6%. Ukuaji huu unachochewa na mazingira bora ya biashara, utalii, na mauzo ya madini. Hii inamaanisha kuwa mzunguko wa fedha upo, na sekta ya fedha ina ukwasi wa kutosha kutoa mikopo na kusaidia miradi ya kimaendeleo.
Siri ya utulivu wa sarafu yetu na uwezo wa kuagiza bidhaa nje ipo kwenye akiba lakini hata hivyo imefikia lengo la kununua tani 20 za dhahabu safi ndani ya miezi 16 tu, ikiwa ni mapema kuliko ilivyotarajiwa. Vilevile, kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayofika Dola bilioni 6.5 (inayotosha miezi 5 ya uagizaji bidhaa) ni "kinga" tosha dhidi ya dhoruba zozote za kiuchumi. Hii inatupa jeuri ya kidiplomasia na kiuchumi duniani
Serikali kupitia BoT imethibitisha kuwa "haijalala." Kupitia bajeti ijayo ya 2026/2027, mikakati zaidi ya kudhibiti athari za nje itawekwa wazi. Ujumbe kwa vijana ni mmoja: msiogope kuwekeza. Mifumo ya malipo ni salama, hakuna udukuzi, na nchi ina akiba ya kutosha. Huu ni wakati wa kutumia utulivu huu wa kiuchumi kubuni mbinu mpya za kibiashara, hususan katika sekta ya nishati mbadala na teknolojia, tukijua kuwa misingi ya nchi imara.

Post a Comment